Portsmouth, Klabu inayochungulia kushuka Daraja kutoka Ligi Kuu huku ikiwa na matatizo kibao ya fedha na ipo hatarini kufilisiwa, leo imetinga Nusu Fainali ya Kombe la FA pale ilipoichapa Birmingham bao 2-0 Uwanjani Fratton Park.
Piquionne ndie shujaa wa Portsmouth alipofunga bao mbili dakika ya 67 na 77 na kupieleka Portsmouth Wembley kucheza Nusu Fainali ya FA Cup.
Mechi nyingine ya Robo Fainali ya Kombe la FA ni baadae leo kati ya Fulham na Tottenham.
Maandalizi ya England Kombe la Dunia
England wamepanga kucheza mechi 2 za majaribio kabla ya kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.
Mechi hizo za majaribio ni dhidi ya Mexico na Japan na zitachezwa mwezi Mei kabla Capello hajateua Kikosi chake cha Wachezaji 23 cha Kombe la Dunia hapo Juni 1.
Capello anategemewa kukitaja Kikosi cha awali hapo Mei 17 kitakachokuwa na Wachezaji 30 na siku hiyo ni siku moja tu baada ya Fainali ya Kombe la FA.
Kambi ya awali ya England inategemewa kuwa Nchini Austria na itafanya mazoezi yake kwa siri.
England inacheza mechi yake ya kwanza kwenye Kundi lake la Fainali za Kombe la Dunia hapo Juni 12 watakapocheza na USA kisha Juni 18 wanacheza na Algeria.
Mechi yao ya mwisho kwenye Makundi ni ile ya Juni 23 na Slovenia.
MAN UNITED HAINUNULIKI!!!
Mkurugenzi Mkuu wa Manchester United, David Gill, amesema uongozi wa Klabu hiyo unaheshimu msimamo wa ‘Wakombozi Wekundu’ [Red Knights] wanaotaka kuinunua Man United kutoka kwa Wamiliki wake wa sasa Familia ya Glazer lakini Gill amesema Klabu hiyo haiuzwi.
Mbali ya ‘Wakombozi Wekundu’ ambao ni Kikundi cha Watu Matajiri Mashabiki wa Manchester United, kuna Kikundi kingine cha Masapota kinachoitwa MUST [Manchester United Supporters Trust] ambacho pia kinataka Familia ya Glazer ing’oke Manchester United.Vikundi hivyo viwili, Red Knights na MUST, vimesema vitakusanya nguvu zao kwa pamoja ili kushinda vita yao.
Inasadikiwa kuwa MUST sasa imefikisha idadi ya Watu 100,000 kwenye safu yao.
Lakini, kuna Wataalam wa ishu za ununuzi wa Makampuni ambao wametoa sababu 5 zitakazofanya Red Knights na MUST kushindwa kuwatoa kina Glazer.
Nazo ni:
BEI: Manchester United ina deni la zaidi ya Pauni Milioni 700.
Familia ya Glazer waliinunua Man United kwa dau la Pauni Milioni 272 na lazima watataka kupata faida ya pesa zao. Hivyo inakisiwa dau la ununuzi litakuwa Pauni Bilioni 1 na nusu na bei hiyo huenda ikawafanya kina Glazer kukubali kukaa mezani na kuzungumzia biashara hiyo.
MFUMO: Red Knights wanataka kuwakusanya Wawekezaji 40 kila mmoja akitoa Mamilioni ili kuinunua Manchester United.
Kwa sababu ni kundi kubwa huenda kukatokea misuguano na kufanya azma yao isifanikiwe.
MENEJIMENTI: Hata kama Red Knights watafanikiwa kuinunua Manchester United kuiendesha Klabu hii kubwa kutakuwa tatizo kubwa hasa ukizingatia Wawekezaji wake ni wengi. Kina Glazer wana Menejimenti nzuri mno huku masuala yote ya mechi na Wachezaji yakiwa chini ya Sir Alex Ferguson na mafanikio yake ni makubwa mno.
Kwa upande wa masuala ya biashara, Klabu hiyo inaendeshwa wakiwa na Ofisi mbili moja Mjini London na moja ikiwa Manchester na Ofisi hizo zimekuwa zikizalisha pesa kwa faida.
GLAZER: Familia ya Glazer imesema Manchester United haiuzwi na hawana presha yoyote ya kuuza.
Pia walipouza Hati za Dhamana hivi karibuni zimesaidia sana kukusanya mtaji wa kulipia deni na kumewafanya kina Glazer waidhibiti vizuri Klabu hiyo.
UTANGULIZI: Haijawahi kutokea kwa Masapota wa Klabu kuichukua Klabu ya Ligi Kuu ingawa kwenye Ligi za chini imeshatokea pale Kabu za Exeter City, Notts County na York City ziliponunuliwa na Mashabiki.
Mashabiki wa Liverpool mwaka jana waliunda Kikundi kinachoitwa Share Liverpool ili kuiteka Klabu hiyo kutoka kwa Wamiliki wake Wamarekani wawili lakini walishindwa kuitwaa.
No comments:
Post a Comment