Sunday 7 March 2010

Goli la 100 la Scholes laipaisha Man United kileleni!!
• Wolves 0 Man United 1
• Arsenal 3 Burnley 1
• West Ham 1 Bolton 2
Kiungo Veterani Paul Scholes jana alifunga goli lake la 100 katika mechi za Ligi Kuu na kuifanya Manchester United iongoze Ligi walipopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolves Uwanjani Molineux.
Bao hilo la Scholes lilifungwa dakika ya 73 na kuifanya Man United iwe na pointi 63, Chelsea na Arsenal zina pointi 61 kila mmoja lakini Chelsea ana tofauti ya magoli bora.
Hata hivyo Chelsea wikiendi hii hawana mechi ya Ligi Kuu kwani wanacheza Robo Fainali ya FA Cup leo na Stoke.
Jana Manchester United ilicheza bila ya mtambo wao wa magoli Wayne Rooney aliepumzishwa kwa vile anasumbuliwa na maumivu ya goti.
Awali Arsenal waliifunga Burnley bao 3-1 uwanjani Emirates na kuwafanya bado wawe tishio kwenye Ubingwa wa Ligi Kuu.
Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 11 kupitia Fabregas.
Kipindi cha pili, dakika ya 50, David Nugent alisawazisha kwa Burnley baada ya kumvika kanzu Kipa Manuel Almunia.
Winga Theo Walcott alipachika bao la pili kwa Arsenal na Mchezaji alieingia toka benchi Andrey Arshavin akaweka bao la 3 dakika za majeruhi.
Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu, Bolton iliweza kujinasua kidogo toka chini baada ya kupata ushindi wa ugenini walipoifunga West Ham bao 2-1.
Bolton walicheza dakika 18 za mwisho wakiwa mtu 10 baada ya Kiungo wao Tamir Cohen kupewa Kadi 2 za Njano na hivyo kutolewa kwa Kadi Nyekundu.
Bolton walipata bao la kwanza dakika ya 11 mfungaji akiwa Kevin Davies na bao la pili lilifungwa na Jack Wilshere, ambae yupo Bolton kwa mkopo kutoka Arsenal.
FA CUP: Fulham 0 Tottenham 0
Katika mechi ya Kombe la FA ya Robo Fainali huko Craven Cottage, Fulham na Tottenham zilitoka sare ya kutofungana na itabidi zirudiane huko White Hart Lane ili kupata Timu moja itakayoenda Nusu Fainali.
Leo kuna mechi mbili za Robo Fainali kati ya Chelsea v Stoke na Reading v Aston Villa.

No comments:

Powered By Blogger