Saturday 13 March 2010

LIGI KUU: Wikiendi hii, Chelsea awania kutwaa uongozi
Tottenham Hotspurs v Blackburn Rovers
Hii ni mechi ya kwanza kwa wikiendi hii na inchezwa mapema kupita zote.
Tottenham, walio nafasi muhimu sana ya 4 ambayo ni ya mwisho kufuzu kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI wapo nafasi hiyo wakiwa pointi sawa na Manchester City ila wamewazidi magoli, wanaikaribisha Blackburn Rovers Uwanjani White Hart Lane.
Blackburn wanaonekana wameshajinasua kutoka balaa la kushushwa Daraja lakini wana rekodi mbaya wakicheza ugenini na mechi ya mwisho kushinda ugenini ilikuwa Novemba mwaka jana.
Chelsea v West Ham
Chelsea wanawakaribisha jirani zao wa London West Ham Uwanjani Stamford Bridge na ushindi kwa Chelsea utawapa tena uongozi wa Ligi Kuu na kuwa pointi moja juu ya Manchester United.
Katika mechi ya mwisho ya Ligi, Chelsea walitandikwa na Manchester City 4-2.
Kwa West Ham, mambo ni mazito kwani wapo 3 tu juu ya Timu zile tatu za mwisho na wamefungwa mechi zao mbili za mwisho.
Burnley v Wolves
Hii ni mechi kubwa kwa Timu hizi kwani Burnley wapo nafasi ya 18, wakiwa moja ya Timu 3 zilizo nafasi ya hatari ya kushushwa Daraja, na Wolves wapo nafasi ya 17.
Burnley hawajashinda katika mechi 5 na Wolves wamefungwa mechi zao 3 za mwisho.
Hii ni mechi inayozikutanisha Timu iliyofunga magoli machache kwenye Ligi [Wolves, goli 21 katika mechi 28] na Timu iliyofungwa goli nyingi [Burnley, goli 61 katika mechi 29].
Bolton v Wigan
Ni pointi moja tu iliyo kati ya Timu hizi lakini Wigan wanaingia kwenye mechi hii wakiwa na furaha baada ya juzi kuitungua Liverpool 1-0 kwenye Ligi.
Nao Bolton wanatoka kwenye kipigo cha 4-0 walichopewa na Sunderland siku ya Jumanne kwenye Ligi Kuu.
Hull City v Arsenal
Arsenal ambao wako nafasi ya 3 wanasafiri hadi KC Stadium kucheza na Hull City ambao wako nafasi ya pili toka mwisho.
Kwa Arsenal, mechi hii ni muhimu kwani ushindi utawafanya waipite Man United ambao wanacheza Jumapili.
Stoke City v Aston Villa
Aston Villa wamecheza mechi 3 pungufu ya Timu zile zinazowania nafasi ya 4 kwa vile wamekuwa na mechi za Vikombe mbalimbali na ushindi kwao ni muhimu ili kuifukuzia nafasi hiyo ya 4.
Stoke wapo nafasi ya 11 na wamefungwa mechi moja tu mwaka huu.
Birmingham v Everton
Wakiwa kwao Uwanja wa Mtakatifu Andrew, Birmingham wanautafuta ushindi wao wa 3 mfululizo kwenye Ligi watakapocheza na Everton ambao wako pointi mbili nyuma ya Birmingham.
Manchester United v Fulham
Hii ni mechi inayochezwa Jumapili na inazikutanisha Timu ambazo mechi zao za mwisho zilikuwa ni za Ulaya wakati Man United walipoitwanga AC Milan 4-0 kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI na Fulham walipopigwa 3-1 na Juventus kwenye EUROPA LIGI.
Mechi ya mwisho ya Ligi kati ya Timu hizi, huku Man United ikiwa haina Difensi na kuwalazimu kuwachezesha Darrren Fletcher na Michael Carrick kama Masentahafu, Fulham walishinda 3-0.
Sunderland v Manchester City
Katika mechi yao ya mwisho, Sunderland waliifunga Bolton 4-0 huo ukiwa ushindi wao wa kwanza katika mechi 15 na kuwainua kuwa pointi 6 mbele ya zile Timu 3 za mkiani.
Man City wao wapo lile kundi linalogombea nafasi ya 4 na wamecheza mechi moja pungufu ya Timu ya 4 Tottenham huku wakiwa na pointi sawa.
Mechi ya mwisho, Man City walipata ushindi wa kishindo walipoichapa Chelsea 4-2 huko Stamford Bridge.

No comments:

Powered By Blogger