FIFA yaipiga buti teknolojia!!!
Dunia ya Soka itaendelea kuutegemea uamuzi wa Binadamu pekee ili kuamua kama mpira umevuka mstari wa goli au la na hivyo ni goli au siyo badala ya kutegemea teknolojia ya kisasa inayotumia mikanda ya video na elktroniki nyingine kutoa uamuzi wa papo kwa papo na sahihi.
Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya Soka [IFAB=International Football Association Board] imepiga kura na kutupilia mbali mapendekezo mawili ambayo yangeondoa kumtegemea Refa tu kutoa uamuzi katika hali za utatanishi kwenye mechi.
Jerome Valcke, Katibu Mkuu wa FIFA, ametamka: “Huu ni mwisho wa kufikiria kutumia teknolojia!”
FIFA imekuwa kwenye shinikizo kubwa la kukubali kutumia teknolojia ya kisasa ili kuondoa makosa makubwa yanayofanywa na Marefa katika mechi kubwa.
Dunia itakumbuka hivi majuzi Republic of Ireland ilivyopokwa kuingia Fainali za Kombe la Dunia pale Thierry Henry wa Ufaransa alipokontroli mpira kwa mkono bila Refa kuona na kumpasia William Gallas alieisawazishia Ufaransa bao na kuiingiza Fainali za Kombe la Dunia.
Valcke amesema uamuzi wa kumwongezea mamlaka Refa wa Akiba [Refa wa nne] ambae huwepo pembeni kwenye kila mechi na pia kuwepo kwa Marefa wengine wasaidizi wawili mmoja nyuma ya kila goli, utafanywa kwenye Kikao maalum cha IFAB mwezi Mei.
IFAB ilianzishwa mwaka 1886 na ndio inayojulikana kama “Mlinzi wa Sheria za Soka” na Wanachama wake ni Vyama vya Soka vya England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini na kila mmoja huwa ana kura moja.
FIFA, katika mikutano ya IFAB, ina kura 4 na ni lazima zipatikane asilimia 75 ya kura zote ili uamuzi kufikiwa.
Nchi za England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini ndizo zinazotambulika kama kiini cha kuanzishwa Soka duniani.
Nae Jonathan Ford, Kiongozi wa FA ya Wales, amesema utata kwenye Soka ndio unafanya Soka kuvutia na hivyo kuanzisha mijadala na malumbano kuhusu matukio mbalimbali yenye utata kwenye mechi ni sehemu ya Soka inayovutia na kuchangamsha.
Ford amesema: “Makosa ya Marefa ni ya kibinadamu! Na hilo huchangamsha Soka na kuwafanya watu wawe na cha kuzungumza kwenye Mabaa miaka nenda rudi!”
No comments:
Post a Comment