Sunday 7 March 2010

FA CUP: Vila iko Nusu Fainali
Aston Villa leo wakiwa ugenini wamefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la FA licha ya kuwa bao 2-0 hadi haftaimu lakini walibadilika kipindi cha pili na kufunga bao 4 na hivyo kuwabwaga Reading 4-2.
Alikuwa ni John Carew aliekuwa shujaa baada ya kuifungia Villa bao 3.
Bao jingine la Villa lilipachikwa na Ashley Young.
England si wazuri kuchukua Kombe la Dunia
Mkongwe wa England, Geoff Hurst, aliefunga goli 3 mguuni kwake katika Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1966 dhidi ya Ujerumani na kuipa England Kombe hilo kwa ushindi wa bao 4-2, amedai Kikosi cha sasa cha England si kizuri kiasi cha kuwa na uwezo wa kuwa Mabingwa wa Dunia.
Hurst amedai Timu hiyo ina kasoro nyingi zikiwemo za kukosa Mafowadi wazuri ukimtoa Wayne Rooney na kukosa Difensi imara baada ya kuumia Mafulbeki Glen Johnson na Ashley Cole pamoja na kuwa na wasiwasi wa kumkosa Rio Ferdinand anaeandamwa na kuumia mara kwa mara.
Hurst amesema England itafika Nusu Fainali tu kwa Kikosi chao kilichopo na kama ingekuwa Fernando Torres anachezea England pamoja na Rooney alikuwa ana uhakika Timu hiyo ingekuwa kiboko.
Tangu itwae Kombe la Dunia mwaka 1966, England imefika Nusu Fainali ya Kombe hilo mwaka 1990 na kutolewa Robo Fainali mwaka 2002 na 2006.
FIFA: Uhamisho Wachezaji Duniani kudhibitiwa
FIFA imesema itaanzisha njia mpya ya kudhibiti uhamisho wa Kimataifa wa Wachezaji ili kuondoa kasoro nyingi zikiwemo zile za Wachezaji kumilikiwa na Kampuni badala ya Klabu wanazochezea na ununuzi wa Wachezaji hao unaohusishwa kuhodhi pesa kinyume cha sheria.
Utaratibu mpya wa FIFA utatumia njia za elektroniki na unaitwa ‘Transfer Matching System’ [TMS] na hivyo kuondoa utaratibu wa sasa wa kutumia faksi na makaratasi ili kuhamisha Wachezaji na hivyo kuondoa dosari nyingi.
Meneja Mkuu wa TMS, Mark Goddard, amesema: “Mpaka sasa mtindo uliokuwa ukitumiwa ni wa makaratasi kama ilivyokuwa miaka 100 nyuma! Ilikuwa ngumu kufuatilia Wachezaji gani wamehamishwa. Kulikuwa na uhamisho feki, kulikuwa na uuzwaji wa Wachezaji ambao hawapo ili mradi Watu mafisadi wahamishe pesa zao toka Nchi moja hadi nyingine kinyume cha sheria!”
Katika mfumo wa TMS uanaotumia mtandao, ili kukamilisha uhamisho wa Mchezaji inabidi Klabu zinazouza na kununua Mchezaji ziingize kwenye mtandao taarifa zote zinazotakiwa kuhusiana na Mchezaji anaehamishwa zikiwemo ada ya uhamisho, mshahara wa Mchezaji huyo, Wakala wake au Mwanasheria wake na muda wa mkataba wake.
Pia, ada ya uhamisho ni lazima itoke Benki moja kwenda nyingine.
Goddard amesema: “Huu ni mradi mkubwa wa FIFA. Haujabadilisha sheria za uhamisho bali unadhibiti uhamisho na kuondoa kasoro na dosari nyingi.”
Moja ya kasoro hizo ni ile ya Wachezaji kumilikiwa na ‘Watu baki” badala ya Klabu. Mtindo huo ni kitu cha kawaida huko Marekani ya Kusini ambako baadhi ya Wachezaji humilikiwa na Makampuni, Mawakala na hata Mifuko ya Pensheni.
Mfano maarufu ni umiliki wa Mchezaji Carlos Tevez aliechukuliwa na West Ham kutoka Corinthians lakini ikabainika baadae kuwa Corinthians haikuwa ikimmiliki.
West Ham ilipigwa faini ya Pauni Milioni 5.5 Aprili 2007 kwa kukiuka sheria za Ligi Kuu zinazokataza Mchezaji kumilikiwa na Kampuni binafsi badala ya Klabu.
Vilevile, mtindo huu wa TMS utaondoa kesi za madai zinazohusiana na kutolipwa au kutokamilishwa ada ya uhamisho wa Mchezaji kwa vile vitu vyote vitakuwa wazi mtandaoni.
Goddard ameongeza kuwa mtindo huo mpya unarahisisha mno uhamisho wa Mchezaji na akatoa mfano wa Mchezaji mmoja aliehama Klabu moja kutoka England na kwenda Scotland na uhamisho wote ikiwemo kupata kibali cha Kimataifa vilichukua dakika 7 tu na Mchezaji huyo akafanikiwa kuichezea Klabu yake mpya siku hiyo hiyo.

No comments:

Powered By Blogger