Sunday 20 December 2009

BAADA YA VIPIGO: Fergie abaki akiombea Madifenda wake wapone, Benitez abaki kulaumu Refa!!!
Kufuatia vipigo kwenye mechi za LIGI KUU England ambako Klabu kongwe Manchester United ilinyukwa na Fulham 3-0 na Liverpool kubamizwa 2-0 na goigoi Portsmouth hapo jana, Mameneja wa Timu hizo wamesimama na kutoa maoni yao tofauti na yenye hisia tofauti.
Sir Alex Ferguson wa Manchester United, ambayo Difensi yake yote, isipokuwa Ptrice Evra, ni majeruhi na hivyo kulazimika kuwachezesha Viungo Darren Fletcher na Michael Carrick kama Masentahafu, amesema Viungo hawawezi kusimama kwenye ulinzi na anaomba kipigo hicho cha Fulham kisije kikawaathiri kutetea Ubingwa wao.
Pia amesisitiza Timu ya Madaktari wa Manchester United inafanya kila hila ili kuwaponya haraka kina Gary Neville, Edwin van der Sar, Wes Brown, Rio Ferdinand, Jonny Evans, Nemanja Vidic, Rafael na Ryan Giggs kabla jahazi halijaenda mrama.
Nae Rafa Benitez, Meneja wa Liverpool, amebaki kumlaumu Refa aliechezesha mechi waliyopigwa 2-0 na Portsmouth kwa kumpa Kadi Nyekundu Kiungo wake Mascherano huku akisahau Kiungo huyo alikula Kadi hiyo huku Liverpool tayari wako nyuma kwa bao 1-0.
Pia alimlaumu Refa huyo kutokumlinda Staa wake Fernando Torres ambae alidai alikuwa akichezewa vibaya kila mara.

No comments:

Powered By Blogger