Monday 21 December 2009

Baridi na Barafu yasababisha mechi ya leo LIGI KUU kuahirishwa!!
Mechi ya Ligi Kuu England iliyokuwa ichezwe leo Jumatatu Desemba 21 kati ya Wigan na Bolton imeahirishwa kufuatia baridi kali na barafu iliyosababisha baadhi ya barabara na Uwanja wa Wigan uitwao DW kuganda kwa barafu.
Ingawa Wamiliki wa Uwanja huo wa DW, Klabu ya Wigan, wamesisitiza Uwanja wao uko salama na unachezeka, Mamlaka za Polisi na Wasimamizi wa Usalama wa Raia wamesema ni hatari kwa mechi hiyo kuchezwa hasa ikizingatiwa baridi hiyo kali, barafu na hali mbaya za barabara na hivyo kuhatarisha maisha ya Washabiki waliopanga kuhudhuria mechi hiyo.
SKANDALI YA TERRY: Nahodha huyo wa Chelsea adaiwa kupokea hongo!!!
Nahodha wa Chelsea, John Terry, amegubikwa na skandali iliyoibuliwa na Gazeti moja huko England lilotoa mkanda wa video na kudai Nahodha huyo alipokea hongo ili kusuka mpango uliofanikiwa wa Waandishi wa Habari wa Gazeti hilo kutembelea kwa siri Kambi ya Mazoezi ya Chelsea iliyopo eneo la Cobham huko London.
Inadaiwa Terry alipokea Pauni Elfu 10.
Hata hivyo Klabu ya Chelsea, ikiongozwa na Meneja Carlo Ancelotti, imekanusha tuhuma hizo na kusisitiza wana imani kubwa na Kepteni wao.
Mchezaji kukosa Fainali Kombe la Dunia kwa kuogopa Wadudu Mabuibui!!!
Straika Supastaa wa Sunderland na Timu ya Taifa England, Darren Bent, miaka 25, ana tatizo kubwa la kuogopa Mabuibui lakini yuko tayari kupatiwa tiba ya kuondoa woga huo ili tu awepo kwenye Kikosi cha England kitakachokuwa Fainali za Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini ambako kunasifiwa sana kwa kuwa na Mabuibui wengi na wa kila aina wakiwemo wenye sumu kali.
Mwenyewe Bent amesema hachukii Wanyama au Wadudu kwani alishawahi kufuga Nyoka alipokuwa mdogo lakini amekiri Mabuibui ndio humtisha sana na huwaogopa sana.
LIGI KUU ENGLAND: Jana Chelsea chupuchupu!!!
Chelsea imeendelea kuwa kinara wa Ligi Kuu na sasa wanaongoza kwa pointi 4 mbele ya Manchester United baada ya jana kutoka suluhu 1-1 ugenini huko Upton Park walipokutana na West Ham.
West Ham walitangulia kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Diamanti aliefunga kwa penalti kufuatia rafu ya Beki wa Chelsea Ashley Cole lakini Chelsea wakasawazisha kwa penalti tata iliyofungwa na Frank Lampard.
Refa Mike Dean aliamuru mara 3 penalti hiyo ya Lampard irudiwe kufuatia Wachezaji kuingia ndani ya boksi kabla penalti hiyo haijapigwa lakini mara zote hizo 3 Lampard alifanikiwa kufunga.
MATOKEO MECHI NYINGINE ZA JANA:
Everton 1 Birmingham 1
Wolves 2 Burnley 0

No comments:

Powered By Blogger