Wednesday, 23 December 2009

KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA lamtia kinyaa Grant!!!
Meneja wa Portsmouth, Avram Grant, anashangazwa mno na FIFA kuruhusu Kombe la Mataifa ya Afrika kuchezwa Januari na kulazimisha Wachezaji Mastaa wanaocheza Ligi kubwa Ulaya kuziacha Klabu zao zinazowalipa pesa nyingi na kwenda Afrika kwa mwezi mzima.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitachezwa huko Angola kuanzia Januari 10 hadi 31 na Klabu kadhaa za Ligi Kuu England zitawakosa Mastaa wao wanaotoka Afrika.
Portsmouth, Klabu iliyomo mashakani kwani ipo mkiani kwenye Ligi Kuu na pia hairuhusiwi kusajili Mchezaji yeyote kwa vile inakabiliwa na madeni yanayotokana na kushindwa kumalizia kulipia ada za uhamisho za Wachezaji kadhaa iliyowanunua, itawakosa Wachezaji wake kina Aruna Dindane toka Ivory Coast, Kanu toka Nigeria, Nadir Belhadj na Hassan Yebda toka Algeria.
Grant ametamka: “Sijui kwa nini FIFA wanaruhusu hili! Sisi tunawalipa Wachezaji hao pesa nyingi, wao wanakaa nao miezi miwili bure! Wachezaji hao wanatakiwa kujiunga na Timu zao za Taifa wiki 2 kabla! “
Grant amesema ataongea na Timu za Taifa za Wachezaji wake ili kuwaombea wachelewe kujiunga ili angalau wawepo kwenye mechi ya Desemba 30 watakapocheza na Arsenal.
Wenger akata tamaa kuhusu Van Persie!!
Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, amekiri kuwa itakuwa ni bahati kubwa kama Staa wake Robin van Persie atapona enka aliyoumia na kurudi uwanjani kabla msimu haujaisha hapo Mei mwakani.
Wenger amesema: “Ikiwa wewe ni mtu wa matumaini, unaweza ukasema atacheza Aprili lakini ukweli ni kuwa ni pengine ni Mei ndio atarudi! Sitaki kujipa matumaini ya uongo! Bora nisubiri tu na ikitokea akirudi mapema hilo litakuwa kama zawadi!”
Van Persie aliumizwa na Difenda wa Italia Giorgio Chiellini Novemba 14 katika mechi ya kirafiki kati ya Uholanzi na Italia na ikabidi afanyiwe upasuaji kwenye enka yake ili kuunga kamba za musuli zilizokatika.
Arsenal imekitaka Chama cha Soka cha Uholanzi kuwalipa fidia kwa kuumizwa Mchezaji huyo lakini inawezekana malipo hayo yasitolewe kwani kuna makubaliano kati ya FIFA na UEFA kulipa fidia tu kwa Wachezaji wanaoumia kwenye Fainali za Kombe la Dunia na Fainali za EURO Cup na si mechi nyingine zozote.

No comments:

Powered By Blogger