Friday, 25 December 2009

Fergie ashutumu kufukuzwa Hughes Man City!!
Sir Alex Ferguson amefoka na kulaumu jinsi Manchester City walivyomfukuza aliekuwa Meneja wao Mark Hughes na kumteua Roberto Mancini kuchukua nafasi yake na kukiita kitendo hicho kuwa ‘hakikubaliki”.
Ingawa Mark Hughes ameiongoza vizuri Manchester City msimu huu ikiwa imefungwa mechi 2 tu kwenye Ligi Kuu, ikiwa ni idadi ndogo kupita Timu yeyote kwenye Ligi Kuu, na pia kuipeleka Timu hiyo kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Carling ambako watakutana mwezi Januari na Mahasimu wao Manchester United, hayo yote hayakutosha kumnusuru kwenye kibarua chake.
Mameneja wengi, akiwemo Mchezaji mwenzake wa zamani Steve Bruce ambae alicheza pamoja na Hughes Manchester United chini ya Sir Alex Ferguson, wamejitokeza kumtetea Mark Hughes na kuponda kwa sauti kali jinsi alivyofukuzwa.
Manchester City, ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wao Garry Cook, wametetea uamuzi wao wa kumtimua Hughes lakini Ferguson amesema: “Ni vitendo visivyokubalika! Hatujali kama umepoteza mechi 2 au 20, kuna njia ya kuwathamini na kuwatendea binadamu! Nashangaa, Naona Xmas huwafanya Wamiliki wa Klabu kuonyesha tabia zao mbovu! Sijui kwa nini! Asubuhi yote ya Jumamosi, mashine za uvumi zilizagaa kufukuzwa kwa Mark Hughes na bila shaka Mark alisikia hilo! Ni hali mbaya mno kuwa kwenye mazingara hayo huku ukijua mechi ya Jumamosi ni ya mwisho kwako!”
Meneja wa Hull Brown aponda mashitaka ya FA na kusema ni kashfa!!!
Meneja wa Hull City Phil Brown amelaumu Klabu yake kushitakiwa, ikijumuishwa na Arsenal, kwa kushindwa kudhibiti Wachezaji wake kufuatia zogo lililotokea kwenye mechi ya Ligi Kuu wiki iliyopita huko Emirates Stadium ambayo Arsenal walishinda 3-0.
Zogo hilo lilizuka baada ya Samir Nasri wa Arsenal kumkanyaga Richard Garcia wa Hull na ndipo Wachezaji wa pande zote kuzongana na Refa Steve Bennett akawapa Kadi za Njano Nasri na Stephen Hunt wa Hull kwa tukio hilo.
Lakini baadae, wakati Timu zikienda Vyumba vya Kubadilisha jezi, Wachezaji wakavaana tena na kuleta kitimtim.
FA imezipa hadi Januari 13 Klabu hizo kuwasilisha utetezi wao wa mashitaka yao.
Phil Brown amedai Klabu yake isingehusishwa kwenye mashitaka hayo na ni Nasri ndie chanzo cha fujo hizo ambazo alizianzisha alipoona Refa Steve Bennett haoni.
Brown amedai Klabu yake itapinga tuhuma za kuleta fujo.
Keane haondoki Spurs!!!
Harry Redknapp amesema hataki kumuuza Nahodha wake Robbie Keane licha ya kukumbwa na mzozo wa kuongoza Wachezaji wa Tottenham kwenda Dublin, Ireland wiki iliyopita kwenye Pati ya Xmas bila ya ridhaa ya Klabu.
Uvumi ulikuwa umezagaa kuwa Harry Redknapp atamuuza Keane na kumnunua Craig Bellamy kutoka Manchester City lakini Meneja huyo wa Tottenham amekanusha habari hizo.
Uvumi huo uliota mizizi kwa Wadau wengi wakizingatia kuwa katika mechi nyingi za hivi karibuni Redknapp amekuwa akiwachezesha kwa pamoja Jermain Defoe na Peter Crouch na kumtupa benchi Keane lakini Redknapp amesema: “Sitaki kumuuza Keane. Hamna Keane wengi kwenye Soka!”
Hata hivyo Redknapp alidokeza huenda akaingia sokoni dirisha la uhamisho litakapofunguliwa mwezi Januari kwani Wachezaji wake Roman Pavlyuchenko na David Bentley wanang’ang’ania kuhama kwa sababu hawapati namba za kudumu hapo Spurs na hivyo huenda akalazimika kuwauza na pesa zao zikasaidia kununua Wachezaji wengine.
Vilevile, Redknapp alizungumzia kuhusu Mchezaji wao Jamie O’Hara ambae yuko Portsmouth kwa mkopo na kusema kuwa ataongea na Mwenyekiti wake ili waamue kama aendelee kubaki Portsmouth au wamrudishe Tottenham.

No comments:

Powered By Blogger