Thursday 24 December 2009

Liverpool yadidimia, Nahodha Gerrard kiwango chini!!
Wakati kuna dhana kubwa Meneja wa Liverpool Rafa Benitez atatimuliwa wakati wowote, pia kuna imani kubwa Nahodha wao Steven Gerrard kiwango chake kimeporomoka mno.
Gerrard, miaka29, ndie alikuwa injini ya mafanikio waliyopata Liverpool miaka ya hivi karibuni ikiwemo kutwaa Ubingwa wa Klabu za Ulaya mwaka 2005 huko Instanbul na kuichachafya Manchester United katika kinyang’anyiro cha Ligi Kuu msimu uliopita.
Lakini msimu huu huku Liverpool ikisuasua na kupoteza mechi nyingi Ligi Kuu na pia kubwagwa nje ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, kiwango cha Gerrard kimeonekana kushuka wazi wazi na kumfanya hata Benitez kumtaka Nahodha wake abadilike na asijipe presha bali acheze mpira wake wa kawaida.
Angalia nini Steven Gerrard alichovuna katika historia yake ya Soka ukulinganisha na Ryan Giggs:
Steven Gerrard [Ameshinda jumla ya Mataji/Tuzo 12:
FA Cup [2], Kombe la Ligi [2], UEFA CHAMPIONS LEAGUE [1], UEFA Cup [1], UEFA Super Cup [2], Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka, toka kwa Waandishi, [1], Mchezaji Bora wa PFA [Chama cha Wachezaji wa Kulipwa [1], Mchezaji Bora Chipukizi wa PFA [1], Mchezaji Bora wa UEFA [1]
Ryan Giggs [Ameshinda Mtaji/Tuzo 27]:
LIGI KUU [11], FA Cup [4], Kombe la Ligi [3], UEFA CHAMPIONS LEAGUE [2], UEFA Super Cup [1], Klabu Bingwa Duniani [2], Mchezaji Bora wa BBC [1], Mchezaji Bora wa PFA [1], Mchezaji Bora Chipukizi wa PFA [2]]
Wenger: “Giggs ni chaguo langu la Mchezaji Bora katika miaka 10!!”
Hivi karibuni Ryan Giggs alipewa Tuzo ya BBC [Shirika la Utangazaji Uingereza] ya kuwa Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2009 na Klabu yake Manchester United ikamwongezea Mkataba ambao utamweka Old Trafford hadi 2011.
Akiwa na umri wa miaka 36, Giggs ndie Mchezaji pekee wa LIGI KUU England aliepata mafanikio makubwa. Giggs ameshashinda Mataji 11 ya Ubingwa wa Ligi Kuu, ametwaa Vikombe vitatu vya Kombe la FA, Vikombe vitatu vya Kombe la Ligi, ameshinda Klabu Bingwa Ulaya mara 2, UEFA Super Cup mara moja na Klabu Bingwa ya Dunia mara 2.
Mafanikio yote ameyapata akiwa na Klabu yake Manchester United ambayo alianza kuichezea tangu akiwa na miaka 14.
Mafanikio yake ni listi ndefu inayozidi kuongezeka.
Giggs ni Mchezaji pekee wa Manchester United kucheza Misimu yote 11 ambayo Man U alitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu. Ni Mchezaji pekee wa Man U aliefunga magoli katika Misimu 11 ya kucheza katika Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Ni Mchezaji pekee kwenye Ligi Kuu kucheza kila Msimu na kufunga katika kila Msimu tangu Ligi Kuu ilipoanza.
Ni Mchezaji wa Pili wa Kiungo katika Ligi Kuu aliefunga zaidi ya Magoli 100 wa kwanza akiwa ni Matt Le Tissier aliekuwa akichezea Southampton.
Arsene Wenger amebaini: “Ryan Giggs ni Mchezaji Bora Ligi Kuu katika kipindi cha Miaka 10 iliyopita! Yeye ana staili na ni Mshindi! Lakini lile goli alilotufunga kwenye Nusu Fainali ya Kombe la FA mwaka 1999 bado linaniumiza roho!!”
LIVERPOOL: Hofu ya kutimuliwa Benitez, Wachezaji waaanza kumtetea!!
Rafa Benitez amekalia kuti kavu hasa baada ya Liverpool kubwagwa nje ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na pia kufanya vibaya kwenye LIGI KUU England wakiwa wameshinda mechi 3 tu kati ya 12 walizocheza mwisho na hivyo kuwa nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi.
Ingawa inaaminika kibarua chake kiko salama kwa sababu tu Liverpool hawana uwezo kifedha kumfukuza na kuteua Meneja mpya kwa kuwa wanakabiliwa na lundo la madeni, hali ni mbaya Klabuni kiasi cha kufanya Wachezaji kujitokeza na kuanza kunadi utetezi wake.
Nyota wa Liverpool, Fernando Torres, amesema: “Kumfukuza Meneja si jawabu! Meneja hachezi, ni sisi inabidi tucheze vizuri pamoja!”
Nae Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, akiunga mkono hoja hiyo, amesema: “Sisi ni timu! Ni sisi wa kulaumiwa kwa hali tuliyonayo!”
Liverpool, inayomilikiwa na Matajiri wa Kimarekani George Gillet na Tom Hicks, inadaiwa Pauni Milioni 240 na endapo watashindwa kufuzu kucheza UEFA CHAMPIONS LEAGUE msimu ujao watakosa mapato ya zaidi ya Pauni Milioni 20.
Hali ya Rafa Benitez imezidishwa ugumu kwa vile hana pesa za kununua Wachezaji ili kuimarisha Kikosi na ili afanye hivyo ni lazima auze baadhi ya Wachezaji ingawa Fernando Torres na Steven Gerrard hawauzwi.
Wachezaji ambao wanadhaniwa watapelekwa sokoni ni Ryan Babel, Andrea Dossena, Andry Voronin na Philipp Degen.
Na endapo watafaulu kuuza Wachezaji, inasemekana Liverpool wanawawinda Luca Toni kutoka Bayern Munich na Ruud van Nistelrooy toka Real Madrid.
Wakati huo huo, Mlinzi wa Liverpool, Glen Johnson, huenda akahojiwa na Polisi baada ya Mwanafunzi mmoja kudai alishambuliwa nje ya Naitiklabu moja Jijini London.
Arsenal na Hull City kitanzini FA!!!
Klabu za Arsenal na Hull City zimeshitakiwa na FA, Chama cha Soka England, kwa kushindwa kuwadhibiti Wachezaji wao kufuatia mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Emirates wikiendi iliyopita ambayo Arsenal walishinda 3-0.
Shitaka hilo linafuatia mzozo uliotokea baada ya Mchezaji wa Arsenal Samir Nasri kumkanyaga Kiungo wa Hull Richard Garcia na kundi la Wachezaji wa pande zote mbili kuvaana baada ya tukio hilo.
Refa Steve Bennett aliwapa Kadi za Njano Nasri na Stephen Hunt wa Hull kufuatia mzozo huo lakini vurugu ziliendelea wakati Wachezaji walipokuwa wakitoka Uwanjani kuelekea Vyumba vya kubadilishia jezi.
Msimu uliokwisha Timu hizi pia ziligubikwa na mzozo baada ya Hull City kudai Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, ambae hakucheza siku hiyo ya tukio kwenye mechi ya Kombe la FA, alimtemea mate Meneja Msaidizi wa Hull lakini uchunguzi wa FA ulishindwa kuthibitisha tukio hilo na hivyo Fabregas hakuchukuliwa hatua yeyote.
Arsena na Hull City zimepewa hadi Januari 13 kujibu mashitaka hayo.

No comments:

Powered By Blogger