Friday 25 December 2009

LIGI KUU England: Tathmini Mechi za Boksingi Dei na za Jumapili
Timu za Ligi Kuu England, baada ya kusheherekea Xmas, hawana nafasi ya kufungua zawadi zao Siku ya Boksingi Dei kwani Klabu 16 zitakuwa kazini siku hiyo na siku inayofuatia Klabu 4 zilizobaki nazo pia zinaingia mtamboni.
RATIBA:
Jumamosi, 26 Desemba 2009
[saa 9 dak 45 mchana]
Birmingham v Chelsea
[saa 10 jioni]
Fulham v Tottenham
West Ham v Portsmouth
[saa 11 jioni]
Burnley v Bolton
[saa 12 jioni]
Man City v Stoke
Sunderland v Everton
Wigan v Blackburn
[saa 2 na nusu usiku]
Liverpool v Wolves
Jumapili, 27 Desemba 2009
[saa 10 na nusu jioni]
Arsenal v Aston Villa
[saa 1 usiku]
Hull v Man U
Baada ya malamiko na kukerwa kwa kutimuliwa kwa Mark Hughes huko Manchester City, Meneja mpya wa Klabu hiyo Mtaliana Roberto Mancini ataanza kibarua chake kwa kuikaribisha Stoke City Uwanja wa City of Manchester hapo kesho.
Mechi nyingine ya kesho ambayo italeta ushindani wa nguvu ni ile itakayozikutanisha Timu za mkiani West Ham ambayo itaikaribisha Portsmouth Uwanjani Upton Park. Katika mechi zao za mwisho Timu hizi zilizo mashakani zilijitutumua na kupata mafanikio mazuri pale Portsmouth walipoitandika Liverpool 2-0 na West Ham kwenda sare na vinara wa Ligi Chelsea kwa bao 1-1.
Birmingham City, walio nafasi ya 7 kwenye Ligi baada ya kutofungwa katika mechi 9 za mwisho, wanawakaribisha Chelsea ambao siku hizi za hivi karibuni wameonyesha kupwaya mno baada ya kushinda mechi moja tu katika 6 walizocheza mwisho. Chelsea huenda wakalazimika kumchezesha Chipukizi Daniel Sturridge baada ya Anelka kuumia na pia kumpa uzoefu kwani hii ni mechi ya mwisho kwa Didier Drogba kucheza kabla hajaenda kwao kujiunga na Timu ya Taifa ya Ivory Coast inayojitayarisha kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Liverpool ambao wako kwenye wakati mgumu kufuatia matokeo mabaya wanawakaribisha Wolves Uwanjani Anfield huku Benitez akisakamwa na kutetewa na Wachezaji wake asifukuzwe. Benitez mwenyewe ameshatangaza ni lazima washinde mechi hii.
Kimbembe kipo kwenye Dabi ya Timu za London huko Craven Cottage wakati Fulham watakapowakaribisha Tottenham, Timu iliyo nafasi ya 5. Kwa sasa Fulham wana matumaini makubwa hasa baada ya kuwaangushia Mabingwa Watetezi Manchester United kipigo cha 3-0 kwenye mechi yao ya mwisho.
Mechi ya Sunderland v Everton ni mechi muhimu mno kwa Klabu hizo kwa vile zote zinasuasua huku Sunderland wakiwa wameshinda mechi 2 tu-dhidi ya Arsenal na Liverpool- katika mechi zao 11 za mwisho na Everton hawajashinda mechi yeyote katika 6 walizocheza mwisho na sasa wako pointi 2 tu juu ya Timu zilizo eneo la kuporomoka Daraja.
Bolton watafanya safari fupi kuelekea East Lancashire Uwanjani Turf Moor kukumbana na Timu ambayo ni ngumu Uwanjani hapo, Burnley, waliofungwa mechi moja tu kati ya 9 za Ligi Kuu Uwanjani hapo. Hata hivyo, bila shaka, Bolton watakuwa wanajiamini hasa baada ya kuifunga West Ham kwenye mechi yao ya mwisho na pia kupata mapumziko ya siku 11 baada ya mechi yao ya Jumatatu iliyokwisha waliyokuwa wacheze na Wigan kuahirishwa kwa sababu ya hali ya hewa ya baridi kali na barafu.
Wigan v Blackburn ni mechi nyingine ngumu inayozikutanisha Timu zenye tofauti ya pointi moja tu kati yao.
Jumapili itaanza kwa mechi kubwa kati ya Arsenal v Aston Villa.
Kimsimamo Arsenal wako nafasi ya 3 na Villa wako nafasi ya 4. Villa hawajawahi kufungwa Uwanja wa Emirates na katika mechi kama hii msimu uliokwisha, Villa waliifunga Arsenal.
Mechi hii itaikutanisha Fowadi ya Arsenal inayofunga Magoli kemkem, Magoli 44 katika mechi 17, na Difensi ngumu ya Aston Villa, iliyofungwa Goli 14 tu katika mechi 18.
Mechi ya pili na ya mwisho siku ya Jumapili ni kati ya Hull City na Manchester United Uwanjani KC. Mabingwa Watetezi, Man U wanaokabiliwa na matatizo ya Difensi kufuatia kujeruhiwa Madifenda wao wote [isipokuwa Evra], wanatoka kwenye kipigo cha 3-0 walichopewa ugenini na Fulham. Hull City nao wana hali mbaya huku wakiwa nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi.
Mvuto kwenye mechi hii ni Refa Alan Wiley [pichani] kupangiwa kuichezesha ikiwa ni mechi yake ya kwanza kwa Man U tangu Meneja wa Man U, Sir Alex Ferguson, kumbatukia hayuko fiti kuchezesha, kauli aliyoitoa mara baada ya sare ya 2-2 kati ya Man U na Sunderland mwezi Oktoba.
Kauli hiyo ilimfanya Ferguson afungiwe mechi 2 na FA licha ya kumwomba msamaha Refa Alan Wiley.

No comments:

Powered By Blogger