Thursday 14 May 2009

Manchester United wala Kiporo, sasa pointi moja tu kuwa Bingwa!!! Je Arsenal kuwapa Ubingwa Old Trafford Jumamosi??

Mabingwa Watetezi wa LIGI KUU England, Manchester United, jana wakiwa wageni wa Wigan ndani ya JJB Stadium kwenye mechi yao kiporo walilazimika kucheza kwa ziada na nguvu zote ili kwanza kuishinda hali ngumu ya mchezo kwani mvua kubwa ilikuwa ikinyesha na Wachezaji kuteleza ovyo na pili kupigana kuwamudu na kuwashinda Wapinzani wao Wigan waliochachamaa vilivyo.

Baada ya kuwa nyuma kwa bao moja mpaka hafutaimu kwa bao lililofungwa na Mshambuliaji wa Wigan Hugo Rodallega kutoka Colombia dakika ya 28 baada ya Vidic kuteleza ndani ya boksi na Rodallega kufumua shuti pembeni wavuni, Man U waliibuka kipindi cha pili na kufunga bao 2. Tevez, alieingizwa dakika ya 58 kumbadilisha Anderson alipachika bao tamu kwa kisigino dakika ya 61 lililomhadaa Kipa Kingson kutoka Ghana kufuatia shuti la Carrick. Huku zikiwa zimesalia dakika 4 mechi kwisha Carrick akafunga bao murua baada ya muvu nzuri sana iliyowahusisha Ronaldo na O'Shea upande wa kulia.

Kwa ushindi huo, huku kukiwa kumesalia mechi 2 tu kwa kila Timu ili kumaliza LIGI KUU, Manchester United yuko kileleni kwa pointi 6 mbele akiwa na poiniti 86, Liverpool wa pili pointi 80, Chelsea nafasi ya 3 pointi 77 na Arsenal ni wa 4 pointi 68.

Ili kutwaa Ubingwa kwa mara ya 3 mfululizo, Man U anahitaji poiniti moja tu katika mechi mbili zilizosalia na Jumamosi yuko nyumbani Old Trafford akipambana na Arsenal.

Vikosi vilikuwa;
Wigan: Kingson, Melchiot, Boyce, Bramble, Figueroa, Valencia, Cattermole, Scharner, Brown, N'Zogbia (Mido 82), Rodallega.
Akiba hawakucheza: Pollitt, Edman, Watson, Koumas, De Ridder, Kapo.
Man Utd: Van der Sar, O'Shea, Vidic, Evans, Evra, Carrick, Scholes (Giggs 75), Anderson (Tevez 58), Ronaldo, Berbatov (Park 89), Rooney.
Akiba hawakucheza: Kuszczak, Neville, Nani, Rafael Da Silva.
Watazamaji: 21,286
Refa: Rob Styles
Barcelona washinda Kombe la Mfalme 'COPA DEL REY' na huko Italy Lazio wanyakua Kombe la Italy kwa matuta!
Barcelona jana usiku walikaza kamba kipindi cha pili na kuwabamiza Athletic de Bilbao mabao 4-1 na kutwaaa Kombe la Mfalme wa Spain [pichani] baada ya kuwa suluhu 1-1 na Athletic Bilbao hadi mapumziko.
Bilbao ndio waliotangulia kupata bao lakini Yaya Toure akaisawazishia Barcelona na kipindi cha pili mabao ya Lionel Messi, Bojan Krkic na Xavi yaliwafanya Barcelona kuwa kidedea.
Huko Italy, baada ya mechi kuwa 1-1, penalti zikapigwa na Lazio wakaibuka washindi dhidi ya Sampdoria baada ya kushinda penalti 6-5 na hivyo kutwaa Kombe la Italia.
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, ashinda Tuzo ya Mchezaji Bora ya Waandishi!!!!
Chama cha Waandishi wa Habari wa Soka cha England kimemtunukia Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard Tuzo ya Mchezaji Bora kwa mwaka 2009.
Gerrard amewapiku Wachezaji wa Manchester United Ryan Giggs na Wayne Rooney kutwaa Tuzo ya mwaka huu.
Tuzo hii ilianza kutolewa mwaka 1948 na Gerrard atakabidhiwa Tuzo yake hapo Mei 29 katika Hoteli ya Royal Lancaster mjini London.
Bayern Munich yapata Meneja mpya baada ya kumtimua Klinsmann!!
Vigogo wa Ujerumani, Bayern Munich, ambao hivi karibuni walimtimua Staa wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann kama Meneja wao, wamemteua Mholanzi Louis van Gaal aliewahi kuwa Bosi wa Ajax, Barcelona na Timu ya Taifa ya Holland, kuwa Meneja wao mpya.
Louis van Gaal, miaka 57, kwa sasa ni Meneja wa Klabu ya AZ Alkmaar ya Holland na ndio kwanza tu ameiwezesha Klabu hiyo kutwaa Ubingwa wa Uholanzi msimu huu. Akiwa na Ajax, Van Gaal aliweza kutwaa UEFA CUP mwaka 1992 na UEFA CHAMPIONS LEGUE mwaka 1995 na alipokuwa na Barcelona aliiwezesha Klabu hiyo kutwaa Ubingwa wa Spain mara 2.
Meneja huyu mpya ataanza kazi yake rasmi tarehe 1 Julai 2009.
Bayern Munich msimu uliopita walishinda Ubingwa wa Ujerumani na Kombe la Ujerumani lakini msimu huu wanasuasua na mpaka sasa kukiwa na mechi 2 tu zimebakia kumalizika kwa Bundesliga, Bayern wamefungana na Wolfsburg kwa pointi kileleni.

No comments:

Powered By Blogger