Wednesday 28 October 2009

Blackburn yakumbwa na Homa ya Mafua ya Kitimoto!!!
Bosi wa Blackburn Sam Allardyce anawakimbia Wachezaji wake kwa sababu hajasikii vizuri huku Wachezaji watatu wa Timu hiyo tayari washakumbwa na Homa ya Mafua ya nguruwe.
Jana Sam Allardyce hakukaa kwenye benchi la ufundi la Timu hiyo katika mechi waliyoshinda 5-2 dhidi ya Peterborough ya kugombea Kombe la Carling.
Inasadikiwa kuna Watu watano wameathirika na ugonjwa huo hapo Blackburn na Jumamosi kwenye kipigo cha 5-0 mikononi mwa Chelsea kwenye mechi ya Ligi Kuu Wachezaji wa kutumainiwa Beki Chris Samba na Kiungo David Dunn hawakucheza kwa kuwa wagonjwa na inasadikiwa wameathirika kwa Homa hiyo.
Jumamosi ijayo Blackburn ni wageni wa Mabingwa Manchester United kwenye Ligi Kuu uwanjani Old Trafford.
FA kuchunguza Mashabiki mechi ya Man U!!!
FA, Chama cha Soka England, kitafanya uchunguzi baada ya kutokea fujo za mashabiki kwenye mechi ya Kombe la Carling kati ya Barnsley na Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo Manchester United ambayo Barnsley walifungwa 2-0.
Kufuatia matukio kadhaa ya fujo, FA inasubiri kupokea ripoti kutoka kwa Refa wa mechi hiyo Chris Foy na Mshauri wa Udhibiti wa Watazamaji wa FA aliyekuwepo kwenye mechi hiyo.
Mashabiki 9 waliswekwa ndani na Polsi katika fujo hizo ambazo chanzo chake ni kunyimwa kuuziwa pombe wakati wa haftaimu.
Mashabiki watatu wa Barnsley walivamia uwanja wakati mechi inaendelea lakini walikamatwa.
Refa aliewatwanga Scholes na Rooney Kadi Nyekundu kuchezesha mechi ya Man U v Blackburn Jumamosi!!!!
Inaelekea balaa la Marefa kuwasakama Manchester United tangu Meneja wao Sir Alex Ferguson kutamka Refa Alan Wiley hayuko fiti linazidi kuwaandama kwani Jumamosi wamepangiwa Refa Phil Dowd kuchezesha mechi yao ya Ligi Kuu na Blackburn Rovers uwanjani Old Trafford na Refa huyo anakumbukwa na Man U kwa kuwatoa Wachezaji wawili wao, Paul Scholes na Wayne Rooney, wote katika mechi moja dhidi ya Fulham walipofungwa 2-0 msimu uliopita.
Mabingwa Manchester United wanahisi wanasakamwa na Marefa kufuatia maamuzi yao ya utata hasa mechi na Liverpool na ya jana na Barnsley na hili wanahisi limekuja baada ya kauli ya Ferguson kumponda Refa Alan Wiley.
Kupangwa kwa Refa Phil Dowd kuchezesha mechi hiyo kutawatia wasiwasi Manchester United na kuendelea kuamini Marefa wana kampeni dhidi yao.

No comments:

Powered By Blogger