Friday, 30 October 2009

KESI YA MARADONA FIFA: AFA wawasilisha utetezi FIFA
AFA, Chama cha Soka cha Argentina, kimepeleka ripoti yao FIFA ili uwe utetezi wa Maradona baada ya FIFA kumfungulia uchunguzi kufuatia matusi aliyoyatoa kwenye TV laivu mara baada ya Argentina kuifunga Uruguay 1-0 huko Montevideo, Uruguay Oktoba 14 na kufuzu kuingia Fainali Kombe la Dunia mwakani.
Mwanasheria wa AFA, Hugo Passos, amesema Maradona alikuwa amekasirishwa na Waandishi wa Habari waliomwekea presha kuwa Argentina haitafika Fainali Kombe la Dunia na ndio maana akakasirishwa na kuwatukana mara baada ya kufanikiwa kuiingiza Argentina Fainali.
Endapo FIFA itamtia hatiani Maradona basi anaweza kupigwa Faini na kufungiwa mechi 5 na hilo linaweza kumwondoa asiisimamie Argentina Fainali Kombe la Dunia.
Mwenyewe Maradona amekataa kuomba radhi kuhusu tukio hilo la Montevideo.
Tangu Maradona achukue Ukocha Argentina Novemba 2008 baada ya kujiuzulu Alfio Basile amekuwa na migongano na Wachezaji, Makocha, Waandishi na Wakurugenzi.
Mchezaji Juan Roman Riquelme ambae ni Kiungo Nyota wa Argentina alijitoa kuichezea Argentina kwa sababu ya Maradona na amemsema Kocha huyo ‘haishi kwa kufuata anachokisema’.
Maradona pia aligombana na Carlos Bilardo ambae alikuwa Kocha wa Argentina iliyotwaa Kombe la Dunia mwaka 1986 ambae aliteuliwa na AFA awe Mkurugenzi wa Ufundi wa Argentina ili kumsaidia Maradona na Maradona akatamka Bilardo ni Mzee anaestahili kuvaa suti na tai na kukaa tu kwenye jukwaa la Waheshimiwa na si kumsaidia yeye.
Fergie alaumu England kucheza mechi za kirafiki katikati ya msimu!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema uamuzi wa FA wa kupanga mechi za kirafiki kwa Timu ya Taifa ya England ambayo tayari imeshajikita Fainali za Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini unaziathiri Klabu za Ligi Kuu England ambazo sasa zinakabiliwa na mechi ngumu za Ligi, UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Makombe ya FA na Carling.
Ingawa Ferguson hakuitaja mechi ipi inamkera lakini Wadau wanahisi ni ile mechi ya kirafiki katikati ya Novemba na Brazil ambayo itachezwa Doha, Qatar na hivyo kuwalazimu Wachezaji kusafiri safari ndefu kwenda kuicheza.
Ferguson ametamka: "Kila Klabu inapenda Wachezaji wake wachezee Timu ya Taifa. Hilo ni muhimu kwao na mimi nataka hivyo. Lakini sisi Makocha tunataka ziwe mechi za Kombe la Dunia au Mashindano ya Ulaya na si mechi ya kirafiki katika Nchi ya mbali!”
Blatter aunga mkono dawa ya kuwekea alama Frikiki!
Rais wa FIFA, Sepp Blatter, ameunga mkono matumizi ya dawa ya kupuliza ambayo hutumiwa na Marefa kuweka alama wapi Frikiki ipigwe na wapi Walinzi waweke ukuta wao wa kujihami ambayo sasa iko majaribioni huko Marekani ya Kusini katika Mashindano ya COPA SUDAMERICANA, Kombe lambalo ipo sawa na Mashindano ya EUROPA LIGI huko Ulaya.
CSF, Shirikisho la Soka la Nchi za Marekani Kusini, limebariki utumiaji wa dawa hiyo ya kusprei ambayo huweza kutumika kwenye nyasi orijino au bandia na hata kwenye viwanja vya udongo na ambayo pia haina madhara.
Baada ya kupulizwa na Refa wapi frikiki ipigwe na wapi Walinzi waweke ukuta wao, dawa hiyo hufutika baada ya sekundi 45 hadi dakika 2.
Marefa hukiweka kikopo cha dawa hiyo kwenye mkanda wao wa kiunoni.
Mvumbuzi wa dawa hiyo Pablo Silva amesema CSF ikiridhika dawa hiyo ina mafanikio basi itajaribiwa pia kwenye Mashindano ya COPA LIBERTADORES ambalo ni Kombe sawa na UEFA CHAMPIONS LEAGUE huko Ulaya.
Kwa sasa dawa ya aina hiyo hutumika kwenye Ligi za Brazil, Mexico na Argentina na imeondoa udanganyifu wa kusogeza mpira wakati wa frikiki na pia kuhadaa ukuta uwekwe wapi.

No comments:

Powered By Blogger