Friday 30 October 2009

Wa Bondeni kupiga kambi Majuu!!
Wenyeji wa Kombe la Dunia, Afrika Kusini, watapiga kambi za mazoezi Brazil na Ujerumani ili kujitayarisha na Fainali za mashindano hayo yatakayochezwa Afrika Kusini kuanzia Juni 11 hadi Julai 11, 2010.
SAFA, Chama cha Soka Afrika Kusini, kimesema watakuwa na kambi 4 kwa ajili ya Bafana Bafana.
Kambi ya kwanza ni Januari huko huko kwao wakati Ligi yao itakaposimama ili kuruhusu Wachezaji wao wanaocheza huko nyumbani ambao ni nusu ya Kikosi cha Bafana Bafana wapige kambi ya kujizoeza kucheza kwenye maeneo yenye mwinuko wa juu sana toka usawa wa bahari ambako oksijeni huwa pungufu na hivyo kusababisha Wachezaji kuishiwa pumzi ili kuwazoeza kupata stamina zaidi.
Mwezi Machi 2010 watapiga kambi Brazil na baadae Aprili huko Ujerumani.
Kambi ya nne na ya mwisho itaanza Mei 6, 2010 huko Afrika Kusini ikijumuisha Wachezaji wote na hii ndio itaendelea hadi Fainali kuanza.
Meneja Mkuu wa Bafana Bafana, Sipho Nkumane, amesema mipango yote ilifanywa kabla ya uteuzi wa hivi majuzi wa Kocha toka Brazil Carlos Alberto Prreira lakini mchango wake utakuwa ni muhimu sana.
Bafana Bafana imepangiwa kucheza mechi 4 za Kimataifa katika miezi 6 ijayo ikiwa ni na Japan Novemba 14, Jamaica Novemba 17, Chile Machi 3, 2010 na Jamaica tena Machi 10, 2010.
Nkumane amesema mazungumzo yanaendelea ili Nchi zote mbili za Korea, Kusini na Kaskazini, ambazo zipo Fainali Kombe la Dunia, zicheze na Bafana Bafana Januari, 2010, na mwezi Machi wacheze na Argentina, Costa Rica na Paraguay.
Baada ya uteuzi wa hivi majuzi wa Carlos Alberto Parreira, SAFA ilibidi wawaombe Wadau wa Soka Afrika Kusini wamuunge mkono Kocha huyo baada ya kuonekana kuna upinzani huku wengi wakitaka Mzawa ndie aiongoze Bafana Bafana.
Baada ya Afrika Kusini kuchaguliwa kuwa Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 Parreira aliteuliwa kuwa Kocha wa Bafana Bafana lakini ilibidi arudi Brazil mwaka jana baada ya mkewe kuugua na kumpisha mwenzake Joel Santana ambae alitimuliwa hivi karibuni baada ya matokeo mabaya yakihusu kufungwa kwa Timu hiyo mechi 8 kati ya 9 za mwisho walizocheza.

No comments:

Powered By Blogger