Tuesday 17 November 2009

Japan hailitaki Vuvuzela!!!
Bosi wa Soka huko Japan Motoaki Inukai amesema ataongea na Rais wa FIFA Sepp Blatter ili kulipiga marufuku Vuvuzela kwenye Fainali ya Kombe la Dunia zitakazochezwa huko Afrika Kusini kuanzia Juni 11 hadi Julai 11 mwakani.
Bosi huyo wa Japan alikerwa sana na Vuvuzela baada ya Japan kutoka suluhu 0-0 na Afrika Kusini hapo juzi kwenye mechi ya kirafiki.
Vuvuzela ni utamaduni wa kushabikia kwa Wapenzi wa Soka huko Afrika Kusini na hupulizwa mfululizo kwenye mechi na kitendo hicho kimewafanya Wachezaji, Makocha na Watangazaji kulalamikia kelele zake hasa hali hiyo ilipojitokeza wakati Kombe la FIFA la Mabara lilipochezwa huko Afrika Kusini mwezi Juni mwaka huu.
Wakati huo, Watangazaji wa TV walilalamika matangazo yao hayasikiki na Mchezaji wa Spain, Xabi Alonso, alidiriki kusingizia walifungwa na Afrika Kusini kwa sababu ya Vuvuzela.
Hata hivyo, msimamo wa FIFA mpaka sasa ni kuwa Vuvuzela ni asili na haki ya Watu wa Afrika Kusini.
Kocha wa Japan, Takeshi Okada, alipohojiwa kuhusu dro ya 0-0 na Afrika Kusini Jumamosi iliyopita na maoni yake kuhusu Vuvuzela, alisema: “Labda Afrika Kusini wakicheza soka zuri, Mashabiki wao wataacha kelele!!!”
Benitez: “Akiuzwa Torres, najiuzulu!!!”
Rafael Benitez, Meneja wa Liverpool, amebwata kuwa akiuzwa Fernando Torres bila ya matakwa yake atang’oka.
Kumekuwa na utata Liverpool huku Klabu ikikabiliwa na madeni ya zaidi ya Pauni Milioni 245 na pia mfarakano kati ya Wamarekani wawili Wamiliki wa Klabu hiyo, Tom Hicks na George Gillet, na hivyo kuibuka kwa dhana kuwa njia rahisi ya kupata pesa nzuri na za haraka ni kumuuza Mchezaji wao Staa Torres kwa bei mbaya.
Benitez amefoka: “Sitarajii hilo!! Lakini ikitokea, najiuzulu!!”
Van Persie kutumia dawa za kienyeji ili apone haraka enka!!!
Robin van Persie yupo tayari kutumia kila aina ya tiba ili apone haraka enka aliyoumizwa Jumamosi iliyopita kwenye mechi ya kirafiki kati ya Nchi yake Uholanzi na Italia.
Van Persie amesema atasafiri hadi Serbia ili akatibiwe na Daktari wa Kike anaeganga na kuchua wagonjwa kwa kutumia maji maji ya mfuko wa kizazi wa kina Mama.
Van Persie amesema Daktari huyo alimtibu Mchezaji Kiungo wa PSV Eindhoven Danko Lazovic na alipona haraka na yeye haoni kwa nini asijaribu kwani tiba hiyo haitomuumiza au kumpotezea chochote.
Klabu ya Van Persie, Arsenal, imekadiria Mchezaji huyo hatacheza kwa wiki 6.

No comments:

Powered By Blogger