Tuesday, 17 November 2009

KOMBE LA DUNIA: Mechi ya Misri v Algeria ni uhasama mtupu!!!
Misri na Algeria zinarudiana Jumatano, Novemba 18 huko Khartoum, Sudan ili kupata Mshindi atakaetinga Fainali za Kombe la Dunia mwakani baada ya Misri kushinda 2-0 Jumamosi mjini Cairo na kufanya Timu hizo zilingane kila kitu na hivyo kulazimisha mechi irudiwe uwanja nyutro.
Ingawa uwanjani, kwenye mechi yenyewe ya Jumamosi mambo yalikuwa shwari lakini nje ya Uwanja ni unyama unyama kwa Mashabiki.
Kasheshe ilianza siku Algeria walipotua mjini Cairo na Genge la Vijana kulivurumisha mawe basi la Timu hiyo lililokuwa likiwapeleka Hotelini na kuwajeruhi Wachezaji kadhaa wa Algeria ambao walicheza mechi ya Jumamosi huku wakiwa na bendeji kichwani.
Hata baada ya mechi hiyo vurugu za Washabiki zilitapakaa kila sehemu na hata Nchi za nje ambako kuna Raia wa Algeria na Misri.
Huko Algeria, Ofisi za Shirika la Ndege la Misri zilivamiwa na kuvunjwa na Waandamanaji na baadhi ya Wamisri wanaoishi huko kupigwa. Inasemekana Wamisri wameanza kuondoka huko Algeria kabla ya hiyo mechi ya kesho.
Vurugu za Raia wa Nchi hizi zimeripotiwa hadi Ufaransa.
Huko Dubai ambako kuna jamii kubwa ya Wamisri na Waalgeria, inadaiwa Polisi imetoa onyo kali kwa hao Wamisri na Waalgeria kuacha vurugu.
Kiini hasa cha uhasama kati ya Nchi hizi kinaweza kuwa mechi kati ya Nchi hizi iliyochezwa mwaka 1989 ambayo Misri walihitaji ushindi au suluhu ili waende Fainali Kombe la Dunia huko Italia mwaka 1990.
Hossam Hassan alifunga bao 1 na kuipa Misri ushindi na ndipo balaa likaanza. Algeria wakadai Refa kala rushwa na baada ya mechi hiyo Mchezaji wa Algeria Lakhdar Belloumi akamtwanga chupa Daktari wa Timu ya Misri na kumtoa jicho.
Misri ikamshitaki na kumhukumu Belloumi aende jela ingawa mwenyewe hakuwepo Misri.
Hukumu hiyo imemfanya Belloumi tangu wakati huo aogope kusafiri nje ya Algeria.
Ili kudhibiti fujo huko Khartoum, Serikali ya Sudan imesema itaweka ulinzi wa Polisi 15,000 kwani inategemewa maelfu ya watu kutoka Misri na Algeria watamiminika kwenye pambano hilo kuungana na Raia wengine wa Nchi hizo wanaoishi Sudan.
KOMBE LA DUNIA: Nchi za Ulaya kupata Timu 4 kesho ziakazoenda Fainali!!
Ukiondoa mechi ya Kundi la Afrika ya marudiano kati ya Misri na Algeria inayochezwa Sudan hapo kesho ambapo Mshindi anaingia Fainali, nafasi 4 za mwisho zilizobaki kuingia Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani zitatoka kwenye mechi 4 za Mtoano za Nchi za Ulaya.
Mechi hizo ni za marudiano kati ya: [Matokeo mechi ya kwanza kwenye mabano]
Ufaransa v Republic of Ireland [1-0]
Slovenia v Urusi [1-2]
Ukraine v Ugiriki [0-0]
Bosnia-Herzegovina v Ureno [0-1]

No comments:

Powered By Blogger