Thursday 19 November 2009

ZOZO la Ufaransa v Ireland: Thierry Henry ni ‘MWIZI!!’, Ireland wataka mechi irudiwe!!!
Chama cha Soka cha Ireland, FAI, wamewasilisha malalamiko yao FIFA wakitaka mechi ya jana ya marudiano ya mtoano wa kuamua Timu ipi inaingia Fainali Kombe la Dunia ambayo ilitoka 1-1 na Ufaransa kupita kwa jumla ya Magoli 2-1 wakitaka irudiwe kwa sababu goli la kusawazisha la Ufaransa lililofungwa dakika ya 104 ya muda wa nyongeza huku Ireland wakiongoza 1-0 lilipatikana baada ya Thierry Henry kuumiliki na kuucheza mpira kwa mkono na kumpasia William Gallas aliefunga.
Mechi ya kwanza iliyochezwa huko Ireland, Ufaransa ilishinda 1-0 na jana hadi dakika 90 kumalizika, Ireland ilikuwa imeshinda 1-0 na hivyo kufanya timu hizo kuwa sare 1-1 na ndipo zikaongezwa dakika 30 za nyongeza.
Hata hivyo, FIFA imesema kwa sheria zao ‘uamuzi wa Refa ni wa mwisho”.
Huku zozo hilo likizagaa hadi kwa Wanasiasa wa Nchi hizo wakati Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen, kuitaka FIFA iamue mechi irudiwe na mwenzake wa Ufaransa, Francois Fillon, kujibu kwa kusema Serikali isiingilie masuala ya Soka, Kocha wa Ireland, Giovanni Trapattoni, amesema hategemei mechi kurudiwa kwani uamuzi wa Refa ni wa mwisho.
Henry aungama: 'Nilishika'
Thierry Henry wa Ufaransa ambae jana aliibua mzozo mkubwa baada ya kuumiliki na kuucheza mpira kwa mkono na kumpasia William Gallas aliefunga goli la kusawazisha dakika ya 104 na kuifanya ngoma iwe 1-1 kati ya Ufaransa na Republic of Ireland ameungama na kusema ni kweli aliucheza mpira kwa mkono.
Henry, mara tu baada ya mechi, alisema: “Ntakuwa mkweli! Niliushika mpira! Lakini mimi sio Refa! Niliushika, Refa hakusimamisha. Sasa muulizeni Refa!!”
Nae Mfungaji wa bao hilo, William Gallas, amedai hakuona kama Thiery Henry aliushika mpira.
Kocha wa Ireland, Giovanni Trapattoni, amesema: “Ulaya nzima waliona mkono!! Hata Refa angemuuliza Henry, angeungama! Bora tungetoka kwa penalti!!! Siku zote tunashika bango: ‘tucheze kwa haki’ [Fair Play] sasa ni haya!! Inasikitisha!”
Kocha wa Ufaransa, Raymond Domenech, ambae hapendwi kabisa Ufaransa, amedai: “Sikuona mkono! Nyie Waandishi mnadai kitu mko nje ya uwanja wakati Refa hakuona!”
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ambae ni Mfaransa na alikuwepo kwenye mechi kama Mtangazaji Mtaalam wa Kituo cha TV cha Ufaransa TF1, alibaini: “Ufaransa imeingia Fainali kwa kosa la Refa!”

No comments:

Powered By Blogger