Maradona kifungo miezi miwili!!!
Kocha wa Argentina Diego Maradona amefungiwa na FIFA asijihusishe na Soka kwa miezi miwili kuanzia Novemba 15, 2009 hadi Januari 15, 2010 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa matusi na maneno ya kashfa kwenye mahojiano ya kwenye TV laivu mara tu baada ya ya mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Uruguay ambayo Argentina walishinda 1-0 na kufuzu kuingia Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
Maradona, aliehudhuria kesi hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA huko Zurich, Uswisi leo, pia amepigwa faini ya Pauni 15,000.
Kamati hiyo imesema haikumpa adhabu kali zaidi kwa vile Maradona alionyesha kusikitishwa na kufedheheshwa na vitendo vyake.
Hata hivyo adhabu hiyo haiwezi kuiathiri sana Argentina kwani katika kipindi hicho cha kifungo cha Maradona, Argentina imepangiwa kucheza mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Czech Republic hapo Desemba 16 ingawa mechi hiyo haijathibitishwa.
Capello: “Brazil ndio kidume!”
Kocha wa England Fabio Capello anaamini kuwa Brazil ndio Timu pekee ya kuogopewa kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwezi Juni, 2010.
Brazil jana iliifunga England 1-0 kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa Doha, Qatar na ingeweza kushinda mabao zaidi ya hilo moja baada ya kukosa penalti na pia kuutawala mchezo.
Capello ana imani Brazil wako tofauti kabisa na Timu nyingine na ametamka: “Hii ni mara ya kwanza tumecheza na Timu yenye nguvu, wepesi na kiufundi wako juu sana! Staili yao ni tofauti kabisa na Spain! Spain wazuri kiufundi na wanapasiana pasi nyingi lakini hawana nguvu na ngome yao si nzuri! Tulipocheza na Spain tulipata nafasi nyingi sana za kufunga lakini na Brazil tulipata mbili tu!”
Arsenal yapata pigo: Van Persie aumia!!
Nyota na tegemezi kubwa la Arsenal Robin van Persie huenda akawa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kuumia enka vibaya kwenye mechi ya kirafiki kati ya Uholanzi na Italia hapo jana.
Van Persie, miaka 26, aliumizwa na Mtaliana Giorgio Chiellini dakika ya 10 tu tangu mechi ianze na madaktari wa Uholanzi wamethibitisha kuchanika kwa misuli ya enka ingawa uchunguzi wa kina inabidi ufanywe ili kujua madhara ya kujeruhiwa hiyo enka.
No comments:
Post a Comment