Wednesday 18 November 2009

Vita ya maneno yazidi kuchochea uhasama Mechi ya leo Misri v Algeria!!
Leo, saa 2 na nusu usiku saa za bongo, kwenye Uwanja wa El Merreikh, Mjini Kharoum, Sudan, Misri inarudiana na Algeria kwenye mechi itakayoamua nani atakwenda Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani baada ya Jumamosi Misri kuifunga Algeria 2-0 mjini Cairo na hivyo kulingana kila kitu na kulazimisha mechi hii irudiwe.
Mechi hii imetawaliwa na uhasama wa kihistoria ambao chanzo chake pengine ni mechi ya mechi ya mwaka 1989 kuamua nani anatinga Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1990 zilizochezwa Italia ambayo Misri waliifunga Algeria 1-0 kwa bao la Hossam Hassan na kuwaudhi Algeria waliodai Refa kala rushwa.
Katika mechi hiyo Mchezaji wa Algeria Lakhdar Belloumi alimtwanga chupa Daktari wa Timu ya Misri na kumtoa jicho.
Wiki iliyopita Algeria walipotua Cairo basi lao lilokuwa likiwapeleka Hotelini lilipigwa mawe na Wachezaji kadhaa kuumizwa.
Baada ya mechi ya Jumamosi huko Cairo watu 32 waliumizwa katika vurugu wengi wao wakiwa Washabiki wa Algeria.
Huko Nchini Algeria, Wamisri wamekuwa wakishambuliwa na mali zao kuharibiwa na kusababisha wengi kuondoka Nchini.
Vurugu za Raia wa Nchi hizi mbili zimetapakaa na kuripotiwa hata huko Ufaransa ambako kuna jamii kubwa ya raia hao.
Mechi ya leo huko Khartoum imetawaliwa na vita ya maneno inayochochewa na Viongozi wa Timu hizo huku Mkuu wa Shirikisho la Soka la Algeria kudai vurugu hizo zinachochewa na Viongozi wa Soka Misri.
Hata hivyo, Kocha wa Misri, Hassan Shehata, amepinga lawama hizo na kusema: “Inasikitisha, Soka ni gemu tu lakini kuna watu wanaigeuza vita!”
Serikali ya Sudan imechukua hatua za kuzuia mlipuko uwanjani kwa kupunguza idadi ya Watazamaji uwanjani kutoka 41,000 hadi 35,000 na pia kuwaweka Polisi 15,000 kulinda amani. Vilevile, zimefunguliwa kambi za Washabiki wa Nchi hizo na kuwatenganisha kwa kilomita kadhaa ili wasiingiliane.
Huko Misri, Serikali imejitolea kuwasafirisha kwa barabara hadi Sudan Vijana wa Chini ya Miaka 30 wapatao 2,000 ambao pia watalipiwa gharama zao zote.
Mara ya mwisho kwa Nchi hizi mbili kucheza Fainali ya Kombe la Dunia ni mwaka 1990 kwa Misri na Algeria ilicheza Fainali za 1986.
Oman 0 Brazil 2
Jana kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa Muscat, Oman, Brazil iliifunga Oman mabao 2-0.
Mabao ya Brazil yalifungwa na Nilmar dakika ya 4 na la pili Oman walijifunga wenyewe baada ya Kiungo wao Oman Hassan Ghailani kufanya kosa kipindi cha pili na kujifunga.

No comments:

Powered By Blogger