Sunday 1 August 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Liverpool yatunguliwa na Monchengladbach
Joe Cole leo alicheza Mechi yake ya kwanza kwa Klabu yake mpya Liverpool lakini ikachapwa 1-0 huko Ujerumani na Borussia Monchengladbach iliyokuwa ikisherehekea Miaka 110 kwenye Uwanja wao Borrusia Park.
Leo, Meneja wa Liverpool, Roy Hodgson, alishusha Kikosi chake imara pale Nahodha Steven Gerrard, Jamie Carragher na Glen Johnson walipochezeshwa kwa mara ya kwanza kabisa katika matayarisho yao ya Msimu mpya.
Bao la ushindi kwa Borussia Monchengladbach lilifungwa dakika ya 8 na Karim Matmour, Mchezaji kutoka Algeria, aliemzidi maarifa Beki wa Liverpool, David Ayala aliechezea shilingi chooni.
Chelsea nayo yatunguliwa!
Chelsea, ikiwa na Vigogo wao John Terry na Frank Lampard waliokuwa wakicheza Mechi zao za kwanza, walichapwa 2-1 na Eintracht Frankfurt Uwanja wa Commerzbank-Arena.
Ochs ndie aliefunga bao la kwanza kwa Frankfurt lakini Lampard akasawazisha.
Bao la ushindi kwa Frankfurt lilikuwa la penalti iliyofungwa na Mchezaji wa Kimataifa wa Uturuki Halil Altintop.
Arsenal yatwaa EMIRATES CUP
Leo Arsenal imefanikiwa kuifunga Celtic ya Scotland bao 3-2 na kutwaa Kombe lao wenyewe la Emirates.
Kikombe hiki pia kilishirikisha AC Milan na Lyon ambazo zilitoka sare 1-1 katika Mechi ya awali leo.
Arsenal walijikuta wako mbele kwa bao 3-0 lakini Celtic wakaja juu na kufunga bao mbili na nusura wasawazishe.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Calos Vela, dakika ya 3, Sagna, dakika ya 45 na Samir Nasri, dakika ya 51.
Celtic walifunga kupitia Murphy dakika ya 73 na Sung Yong dakika ya 83.

No comments:

Powered By Blogger