Wednesday 27 August 2008

LEO PATASHIKA KLABU BINGWA ULAYA:
Arsenal v FC Twente
Leo Arsenal wanashuka dimbani uwanjani kwao Emirates Stadium kurudiana na Klabu ya Uholanzi FC Twente ambayo iko chini ya Meneja wa zamani wa Uingereza Steve McClaren katika mechi ya marudiano ya mtoano wa Raundi ya Tatu ya mashindano ya LIGI ya Klabu Bingwa Ulaya maarufu kama UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Katika mechi ya kwanza Arsenal ikicheza ugenini huko Uholanzi ilishinda kwa mabao 2-0 na hivyo leo sare ya aina yeyote ile au wakifungwa bao 1-0 basi wanasonga mbele katika hatua inayofuata ambayo ni ya makundi.
Leo Arsenal wanategemea kumchezesha mchezaji wao kiungo mahiri Cesc Fabregas ambae hajacheza tangu msimu uanze kwani alikuwa majeruhi.
Mchezaji wao mpya Mikael Silvestre waliempata kutoka Manchester United hawezi kucheza kwa sababu ni majeruhi.
Mechi hii inaanza kuchezwa saa 4 dakika 5 usiku saa za bongo.
Liverpool v Standard Liege
Baada ya kuendeshwa puta mechi ya kwanza iliyochezwa Ubelgiji ambayo Kipa wao Pepe Reina aliokoa penalti iliyowafanya Liverpool wanusurike ugenini kwa sare ya 0-0 leo Liverpool wanashuka ngomeni kwao Uwanja wa Anfield wakitafuta ushindi utakaowafanya siku ya Alhamisi wawemo kwenye kapu la timu nyingine za Ulaya zitakapoingia kwenye droo ya kupanga makundi ya LIGI ya KLABU BINGWA ULAYA maarufu kama UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Mechi inaanza saa 4 dakika 5 saa za bongo na inaonyeshwa moja kwa moja na DSTV Supersport 3.

No comments:

Powered By Blogger