Monday 8 September 2008

MCHUJO WA NCHI ZA MAREKANI KUSINI:
BRAZIL WAPAA HADI NAFASI YA PILI!

Leo alfajiri Brazil imepata ushindi mnono wa ugenini baada ya kuwafunga wenyeji wao Chile mabao 3-0 na hivyo kumpa ahueni Kocha wao ambae ni Nahodha wa zamani wa Brazil Dunga kutoka kwenye hatihati ya kumwaga unga katika mechi za mchujo kutafuta timu zitakazoingia Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010.
Ingawa Ronaldinho alikosa penalti mabao mawili ya Luis Fabiano na moja la Robinho yaliwainua Brazil na kuwafanya wachupe toka nafasi ya sita hadi ya pili nyuma ya Paraguay ambao wako pointi mbili mbele.
Nafasi ya tatu inashikwa na Argentina na ya nne ni Uruguay.
Katika kundi hili timu nne za juu zinafuzu kuingia Fainali moja kwa moja na ya tano itacheza na timu kutoka kundi dogo la Marekani ya Kati kupata mshindi.
Jana Argentina wakiwa nyumbani walibanwa na Paraguay kwa kutoka suluhu ya bao 1-1 katika mechi ambayo wachezaji wawili wa Manchester United walikuwa vivutio-ingawa mmoja wa zamani-Gabriel Heinz alijifunga mwenyewe na Carlos Tevez alipata kadi nyekundu.
Pia jana hiyo hiyo Uruguay alimfunga Colombia 1-0 nyumbani kwake.
Mechi za Kundi hili zitaendelea kesho kwa mechi kati ya Paraguay na Venezuela.
Kesho kutwa ni mechi hizi:
Uruguay v Ecuador
Chile v Colombia
Peru v Argentina
Brazil v Bolivia

No comments:

Powered By Blogger