Carvalho: ‘Ni mwaka mbaya sana kwangu!!’
Ricardo Carvalho, Sentahafu wa Chelsea, amesema yuko tayari kuhama Chelsea baada ya kuteseka msimu mzima uliopita kwa kuumia mara kwa mara na kuuita mwaka huo ‘ni mbaya sana kwake!’
Mlinzi huyo toka Ureno mwenye umri wa miaka 31 amezungumza akiwa kwenye Kambi ya Timu ya Taifa ya Ureno inayojitayarisha kwa mechi za mchujo kuwania nafasi za kuingia Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini 2010.
‘Nimekuwa na mafanikio mazuri Chelsea kwa miaka minne,’ Carvalho alisema. ‘Lakini mie niko tayari kwa yeyote atakaenitaka!’
Carvalho amecheza zaidi ya mechi 100 akiwa Chelsea tangu alipotua hapo pamoja na Meneja Jose Mourinho wote wakitokea FC Porto ya Ureno mwaka 2004.
Lakini msimu uliokwisha juzi, msimu wa mwaka 2008/9, Carvalho ameichezea Chelsea mechi 18 tu.
Nahodha West Ham aukataa mkataba mpya!!
Lucas Neill, Nahodha wa West Ham, amekataa kusaini mkataba unaomuongezea mwaka mmoja.
Neill [31], anaetoka Australia, amegoma kusaini mkataba huo wa mwaka mmoja kwa madai kuwa unashusha hadhi na thamani yake kama Mchezaji na Nahodha wa West Ham.
Neill kwa sasa yuko na Timu yake ya Taifa ya Australia itakayocheza mechi 3 dhidi ya Qatar, Bahrain na Japan za mchujo za Kundi la Asia ili kuwania nafasi kuingia Fainali ya Kombe la Dunia Afrika Kusini 2010 na Australia inahitaji pointi moja tu katika mechi hizo 3 ili kutua Afrika Kusini.
Lucas Neill alinunuliwa na West Ham Januari 2007 kutoka Blackburn kwa thamani ya Pauni Milioni 1 na nusu.
Hata hivyo inaelekea West Ham wana nia ya kujijenga upya chini ya Meneja Gianfranco Zola kwani Tovuti ya Klabu hiyo imetaja majina ya Wachezaji 12 tu watakaobaki kwa msimu ujao na nao ni Herita Ilunga, Jack Collison, Mark Noble, Savio Nsereko, Freddie Sears, Junior Stanislas, Marek Stech, James Tomkins, Dean Ashton, Valon Behrami, Carlton Cole na Scott Parker.
Klabu hiyo pia imesema Wachezaji Diego Tristan, Lee Bowyer, Walter Lopez, Kyel Reid, Tony Stokes na Jimmy Walker wote wako huru kuondoka hapo.
No comments:
Post a Comment