Thursday, 4 June 2009

Real mimacho kwa Kaka na Ronaldo
Rais wa Real Madrid Florentino Perez, bila kupoteza wakati tangu alipothibitishwa Rais hapo Jumatatu,, ameanza kampeni zake kwenye vyombo vya habari kwa kutangaza anafanyia kazi ‘kuwabeba’ Kaka na Cristiano Ronaldo ili watue Bernabeu.
Inadaiwa kwa sasa Real Madrid wako mazungumzoni na AC Milan ili wamnunue Kaka lakini habari hizo hizo zinasema hamna mazungumzo ya aina yeyote kati ya Real Madrid na Manchester United ambao msimu uliopita walikataa katakata hata kufikiria kumuuza Ronaldo na ilifika hatua ya wao kuwashitaki Real Madrid FIFA kwa kujaribu kumrubuni Ronaldo kinyume cha taratibu.
Perez amekaririwa akisema: ‘Kaka, Ronaldo na Messi ndio bora duniani! Nitafanyia kazi kuwaleta Kaka na Ronaldo Real!! '
Juzi Jumanne ziliibuka habari kuwa Chelsea wanataka kuiteka nyara dili ya Kaka kwa kutoa ofa ya kitita cha Pauni Milioni 73.3 kumnunua Kaka kutoka AC Milan dau ambalo liliipiku ofa ya Real Madrid ya Pauni Milioni 56 lakini baadae Chelsea wakakanusha taarifa hizo.
Perez akaongeza: ‘Ikiwa Chelsea hawamo kwenye kinyang’anyiro ni nafuu kwetu! Tuna uhusiano mzuri na AC Milan na mimi ni rafiki na Adriano Galliani [Meneja Mkuu AC Milan] na hii itarahisisha kazi yangu.’
Hata hivyo Mmiliki wa AC Milan, Silvio Berlusconi, ambae pia ndie Waziri Mkuu wa Italia, amekanusha taarifa zote za Kaka kwenda Real Madrid na amesema: ‘Hamna uamuzi. Ntakutana na Kaka Jumatatu kasha ntawaambieni nini kitajiri.’
LIGI KUU kuonyesha mechi China, Afrika na India bure!!!
Wamiliki wa LIGI KUU England, wakati wanajitayarisha kwa Mkutano wao Mkuu wa Mwaka, wamedokeza kuwa kuna mipango ya kubadilisha jinsi makubaliano ya kupeperusha matangazo ya mechi laivu yanavyofikiwa na pia kutoa ofa ya kuonyesha baadhi ya mechi zake za laivu bure kwa Watangazaji wa TV China, Afrika na India wenye Stesheni zinazotangaza bure.
Kikao cha Mkutano huo wa mwaka kinachoanza leo kitasimamiwa na Mkurugenzi Mkuu wa LIGI KUU, Richard Scudamore, na Mkuu wake wa Habari na Matangazo, Phil Lines, ndie atatoa mapendekezo hayo mapya.
Hatua hii inakuja kwa kile walichokiita kukabiliana na hatari ya kushindwa na Kampuni za Kimarekani katika vita ya matangazo ya michezo kwenye TV.
Ingawa LIGI KUU imezalisha zaidi ya Pauni Bilioni 2 kwa matangazo ya Msimu wa 2010/11 ambayo tayari yashauzwa na mechi zake za msimu uliopita wa 2008/9 kushuhudiwa katika nyumba Milioni 662 dunia nzima, Wasimamizi hao wa LIGI KUU wamekiri kuwa walifanya kosa kubwa huko China kwa kukubaliana na Kampuni binafsi ya TV iitwayo WinTV ambayo haina soko kubwa kwenye Nchi hiyo yenye Watu wengi sana wakati NBA, Chama cha Mpira wa Vikapu cha Marekani, na Ligi nyingine za Soka kama vile Bundesliga, zinaonyeshwa kwenye TV ya Serikali ya China CCTV ambayo hutazamwa na watu wengi sana huko.
Hiyo ndio sababu kubwa inayowafanya LIGI KUU kutoa ofa ya kuonyesha baadhi ya mechi laivu bure katika Nchi za China na India, zenye watu wengi sana, na Bara la Afrika ambako LIGI KUU ndio nambari wani.

No comments:

Powered By Blogger