Friday, 9 October 2009

FIFA U-20 WORLD CUP EGYPT 2009
Huku Wenyeji Misri wakiwa wamebwagwa nje na Afrika imebaki Nchi moja tu, Ghana, Kombe la Dunia kwa Vijana Chini ya Miaka 20 leo linaingia hatua ya Robo Fainali kwa mechi mbili leo na mechi mbili kesho.
ROBO FAINALI:
09/10/09: South Korea v Ghana
09/10/09: Italy v Hungary
10/10/09: Brazil v Germany
10/10/09: UAE v Costa Rica
NUSU FAINALI:
Oktoba 13:
South Korea/Ghana v Italy/Hungary
Brazil/Germany v UAE/Costa Rica
FAINALI:
Oktoba 16
KOMBE LA DUNIA Afrika Kusini 2010
Wakati kona mbalimbali za Dunia zitawaka moto wikiendi hii na Jumatano ijayo ili kukamilisha Nchi 32 zitakazoingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani zitakazochezwa Juni 11 hadi Julai 11, mpaka sasa ni Timu 11 zifuatazo ndizo tayari zishaingia Fainali hiyo:
South Africa (Wenyeji), Ghana, Australia, Japan, South Korea, North Korea, Brazil, Paraguay, Spain, England na Uholanzi
Ifuatayo ni tathmini ya hali ilivywo katika Makundi mbalimbali kona zote za Dunia.
AFRICA
WALIOFUZU: South Africa [Wenyeji] na Ghana
Kama Wenyeji, Afrika Kusini tayari wako Fainali pamoja na Ghana ambao wamefuzu huku wakiwa na mechi mbili mkononi..
Timu katika kila Kundi zimebakiwa na mechi 2 na Timu ya juu ndio inatinga Fainali.
Cameron wako juu kwenye Kundi lao Kundi A wakiwa na pointi 7 wakifuatiwa na Gabon pointi 6, Togo pointi 5 na Morocco pointi 3.
Kundi B Tunisia yuko juu na pointi 8, Nigeria pointi 6, Mozambique pointi 4 na Kenya pointi 3.
Kundi C, Algeria wanaongoza wakiwa na pointi 10, Egypt pointi 7, Zambia pointi 4 na Rwanda 1.
Kundi D, Ghana mwenye pointi 12 tayari ashafuzu kuingia Fainali huku wakibaki Mali pointi 5, Benin 4 na Sudan 1.
Kundi E ni Ivory Coast mwenye nafasi nzuri akiwa na pointi 12 na anahitaji pointi moja tu katika mechi zake mbili ili aingie Fainali.
Burkina Faso anafuata na pointi 6 huku Guinea na Malawi wakiwa na pointi 3 kila mmoja.
ASIA
WALIOFUZU: Australia, Japan, South Korea na North Korea.
Tayari Australia, Japan, Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini wako Fainali na itapatikana Timu moja nyingine itakayoungana nao baada ya mtoano kati ya Bahrain na New Zealand utakaochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
MAREKANI YA KASKAZINI, KATI NA CARIBBEAN
WALIOFUZU: Bado Kupatikana
Endapo USA na Mexico watashinda mechi moja tu kati ya mbili walizobakiwa nazo watatinga Fainali wakiwaacha Honduras na Costa Rica kugombea nafasi ya 3 itakayowawezesha kutinga Fainali moja kwa moja ingawa El Salvador nao wapo kwenye mahesabu.
Hata hivyo, kwa jinsi hali ilivyo, El Salvador huenda akaambulia nafasi ya 4 na hivyo kwenda kucheza mtoano na Timu itakayomaliza nafasi ya 5 toka Nchi za Marekani ya Kusini.
MAREKANI YA KUSINI
WALIOFUZU: Brazil na Paraguay
Brazil na Paraguay tayari zimetinga Fainali huku wakiwa na mechi 2 mkononi huku Chile, alie nafasi ya 3, akihitaji kushinda mechi moja tu kati ya mbili alizokuwa nazo kuungana nao.
Balaa lipo kwenye nani atachukua nafasi ya 4 ili kuingia Fainali moja kwa moja na ile ya 5 ili kwenda kucheza kwenye mtoano na Timu inayomaliza nafasi ya 4 toka Kundi la Nchi za Marekani ya Kaskazini, Kati na Carribean.
Kukiwa kumebaki mechi 2, Ecuador yuko nafasi ya 4 akiwa na pointi 23, Argentina wa 5 pointi 22, Uruguay na Venezuela wana pointi sawa 21 kila mmoja ila Uruguay yuko mbele ya Venezuela kwa magoli.
Colombia nae ananyemelea akiwa na pointi 20.
ULAYA
WALIOFUZU: England, Spain na Uholanzi
Ni England, Spain na Uholanzi ambazo tayari zimeingia Fainali.
Yapo Makundi 9 na Washindi wa kila Kundi wanatinga Fainali huku Washindi wa Pili Bora wa nane watawekewa droo maalum ili kupanga mechi 4 zitakazochezwa nyumbani na ugenini ili kupata Timu 4 zitakazoenda Fainali.
KUNDI 1: Lipo wazi ingawa Denmark anaeongoza anahitaji pointi 2 toka mechi 2 ngumu dhidi ya Mahasimu wao Sweden na Hungary ili afuzu. Kundi hili lina Ureno pia ambao mpaka sasa wanasuasua ingawa mechi zao zilizobaki wanacheza na Hungary nyumbani [baada ya kuifunga huko Hungary] na Timu dhaifu Albania.
KUNDI 2: Uswisi wako mbele kwa pointi 3 na wana mechi laini kidogo na wachovu Luxemborg. Inaelekea Greece na Latvia zinagombea nafasi ya pili.
KUNDI 3: Slovakia wana hali nzuri kwani wanahitaji kushinda au Slovenia wafungwe ili wafuzu. Czech Republic bado wana nafasi ya kupata nafasi ya pili na hata Poland, kimahesabu, bado ana nafasi hiyo.
KUNDI 4: Ni Germany au Urusi ndie atakaefuzu kuingia Fainali moja kwa moja na Timu hizi zinapambana uso kwa uso huko Urusi katika pambano litakalotoa sura nani Mshindi wa kwanza ingawa Germany ndie alie nafasi nzuri kwani yuko mbele kwa pointi moja.
KUNDI 5: Spain ameshanyakua nafasi ya kwanza Kundi hili na hivyo kuingia Fainali na vita iliyobaki ni nani Mshindi wa Pili ili aende kwenye mtoano wa kuingia Fainali. Kukiwa na mechi 2 zilizobaki, Bosnia-Herzegovina ana nafasi nzuri kwani yuko mbele ya Uturuki kwa pointi 4.
KUNDI 6: England tayari yuko Fainali na wa pili ni Croatia lakini ikiwa Ukraine atashinda mechi zake 2 zilizobaki basi atanyakua nafasi ya pili.
KUNDI 7: Serbia anahitaji ushindi kwenye mechi moja tu kati ya 2 ili afuzu. Ufaransa nae anahitaji kushinda mechi moja ili angalau amalize wa pili ingawa pia Austria nae bado anayo matumaini.
KUNDI 8: Mabingwa Watetezi wa Dunia, Italy, wanahitaji suluhu tu ugenini na Republic of Ireland ili watinge huko Afrika Kusini mwakani kutetea taji lao.
KUNDI 9: Uholanzi walishinda mechi zao zote kwenye Kundi hili na kuingia Fainali na Norway ndie atakaemaliza nafasi ya pili lakini nafasi yao kuingia Fainali kwa kapu la Washindi wa Pili liko finyu kwani wao, katika Washindi wa Pili toka Makundi 9, ni wa mwisho na ni Timu 8 tu ndizo zinazochukuliwa kwenye droo maalum.

No comments:

Powered By Blogger