Wednesday, 14 October 2009

Jino lazua balaa kwa Fellaini!!!
Kiungo wa Everton na Ubelgiji, Marouane Fellaini, yuko kwenye mzozo na Chama cha Soka cha Ubelgiji [KBVB] pamoja na Kocha wa Timu ya Taifa ya Ubelgiji, Dick Advocaat, baada ya kujitoa kwenye Kikosi cha Ubelgiji kilicho kwenye mechi za Mtoano za Kombe la Dunia ambacho Jumamosi kilicheza na Uturuki na leo Jumatano kinapambana na Estonia.
Kocha huyo wa Ubelgiji, Dick Advocaat, mara baada ya mechi ya Jumamosi ambayo Ubelgiji waliifunga Uturuki alimruhusu Fellaini ajitoe Kikosi cha Ubelgiji ili akafanyiwe operesheni ya kung’oa jino la gego lililomsumbua muda mrefu. Lakini, baadae, Kocha huyo alibadili msimamo na kumtaka Fellaini abaki Kambini ili awemo kwenye Kikosi cha kinachopambana na Estonia Jumatano Oktoba 14 mechi ambayo si muhimu kwa Ubelgiji kwa vile haiwezi kuingia Fainali za Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Fellaini aliondoka Kambini na kwenda kutibiwa jino lake.
Kitendo hicho cha Fellaini kimewaudhi KBVB na kimewatumia faksi Everton kuwajulisha watatumia sheria ya FIFA inayowapa uwezo kumpiga marufuku Mchezaji huyo kuchezea Klabu yake kwa siku 5 baada ya mechi inayohusu Nchi yake ambayo amejitoa Kikosini.
Endapo KBVB itamfungia Fellaini kwa siku hizo 5 basi hataweza kuichezea Everton kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi dhidi ya Wolverhampton Wanderers.
Everton imelalamika kuhusu hatua hiyo ya KBVB na kusema wao kama Klabu hawahusiki kwenye mzozo wa Mchezaji huyo binafsi na Nchi yake.
Megson amtetea Fergie!!
Kocha wa Bolton Wanderers, Gary Megson, ambayo Timu yake itapambana na Manchester United kwenye mechi ya Ligi Kuu hapo Jumamosi, amemtetea Sir Alex Ferguson wa Man U katika mzozo unaoihusu kauli ya Ferguson kusema Refa Alan Wiley aliechezesha mechi ya Man U na Sunderland ‘hayuko fiti’ na kusababisha Chama cha Marefa kumjia juu na pia FA kumtaka Ferguson ajieleze.
Megson amesema: “Wanamwandama kwa vile ni mtu mwenye jina kwenye Soka! Ameomba radhi lakini kila mtu analaumu hata huko kuomba radhi kwake! Asingeomba radhi wangemsema, kaomba radhi wanamsema! Sasa afanyeje? Ameomba radhi huo ungekuwa mwisho wa mzozo!”
Mpaka sasa Sir Alex Ferguson binafsi hajazungumza lolote sakata hilo kwa vile yuko safarini huko New York, Marekani.

No comments:

Powered By Blogger