Friday 16 October 2009

Liverpool ipo Sokoni!!!
Mwana wa Kifalme wa huko Saudi Arabia Faisal bin Fahd bin Abdullah inasemekana ametamka Kampuni yake iitwayo F6 ipo kwenye hatua za mwisho za mazungumzo ya kununua hisa za Klabu ya Liverpool na Mikutano hiyo inafanyika huku mmoja wa Wamiliki wawili wa Kimarekani, George Gillett , yupo huko Saudi Arabia.
Ilitangazwa kuwa George Gillett ameenda huko Saudi Arabia ili kujadili mradi wa Liverpool kuuanzisha Vyuo vya Soka huko Arabuni.
Kwa muda mrefu George Gillett na Mmilki mwenzake Tom Hicks wamekuwa wakitafuta Mwekezaji mwingine ili wasaidiwe mzigo mkubwa wa madeni yanayoikabili Liverpool.
Mkuu wa F6, Barry Didato, amekaririwa akisema Mmiliki wa Kampuni hiyo, Mwana wa Kifalme Faisal, alikuwa akitafakari kuinunua Liverpool na anaweza kununua hisa kuanzia “sifuri hadi asilimia mia”.
Hata hivyo Didato amesema Faisal amekuwa akitafakari kwa undani zaidi hasa kutokana na kutokuelewana kati ya Wamiliki hao wawili wa Kimarekani wa Liverpool, Gillett na Hicks, na pia Madeni yaliyoendelea kuongezeka na kuisakama Liverpool tangu Wamarekani hao wainunue Liverpool mwaka 2007.
Robinho aanza kuweweseka?
Mshambuliaji kutoka Brazil, Robinho, amekiri kuwa angependa kuichezea Barcelona lakini mpaka sasa hajapata ofa yeyote kutoka huko Barca.
Robinho alisaini kucheza Manchester City mwaka jana kwa ada ya Pauni Milioni 32 kutoka Real Madrid na ada hiyo ni rekodi kwa ununuzi wa Mchezaji huko Uingereza lakini muda wote mpaka sasa uvumi wa yeye kuhama unamwandama na umezidi kushamiri baada ya Kocha wa Barca Pep Guardiola kuripotiwa akisema angependa kuwa na Mbrazil huyo mwenye miaka 25.
Gazeti la El Mundo Deportivo limemkariri Robinho akisema: “Hakika ntapenda kuchezea Barca! Nani atakataa kucheza huko? Ni furaha kubwa kucheza pamoja na Messi, Mbrazil mwenzangu Dani Alves, Xavi, Iniesta na Ibrahimovic! Barca wanacheza soka tamu kama Timu bora ya Brazil!”
Hata hivyo, Robinho amesema atabaki kuwa na moyo thabiti na Man City kwani bado ni Mchezaji wao.
FIFA U-20 WORLD CUP Egypt 2009:
NI FAINALI: Ghana v Brazil
Ghana wanakutana na Mabingwa mara 4 wa Kombe la Dunia kwa Vijana wa Chini ya Miaka 20, Brazil, kwenye Fainali ya Kombe hilo itakayochezwa Ijumaa Oktoba 16 Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, mjini Cairo, Misri.
Ghana walitinga Fainali baada ya kuifunga kwenye Nusu Fainali Hungary mabao 3-2 na Brazil waliwafunga Costa Rica bao 1-0.
Mwaka 1993, huko Sydney, Australia, Ghana na Brazil zilikutana Fainali na Brazil wakaibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1.
Kikosi cha Ghana kinaongozwa na Kocha Sellas Tetteh na Nahodha wa Timu hiyo ni Andre Ayew, anaechezea Olympique Marseille ya Ufaransa, na ni mtoto wa Abedi Pele, Mchezaji wa zamani na Supastaa wa Ghana na Afrika nzima.
Kikosi cha Brazil kipo chini ya Kocha Rogerio.
VIKOSI:
Ghana:
Daniel Agyie, Robert Dabuo, Joseph Addo, Samuel Inkoom, Jonathan Mensah, Daniel Addo, David Addy, Ghandy Kassenu, Daniel Opare, Philip Boampong, John Benson, Bright Addae, Gladson Awako, Abeiku Quansah, Emmanuel Agyemang-Badu, Andre Ayew, Mohammed Rabiu, Latif Salif, Ransford osei, Dominic Adiyah
Brazi:
Rafael, Renan Ribeiro, Saulo Douglas, Dalton, Rafael Toloi, Renan, Diogo, Paolo Henrique, Fabricio, Wellington Junior, Bertucci, Alex Teixeira, Maylson, Giuliano, Douglas Costa, Souza, Boquita, Alan Kardec,
Kroenke aongeza kasi ya ununuzi hisa Arsenal!!!
Mmarekani Stan Kroenke ambae ni Mkurugenzi wa Arsenal na vile vile Mmilikiwa wa Hisa za Klabu ya Arsenal ameongeza kasi ya ununuzi wa Hisa zaidi na sasa anamiliki Hisa Asilimia 28.9.
Kufuatana na Sheria za Masoko huko Uingereza, Kroenke akifikisha kumiliki idadi ya Asilimia 29.9 ya Hisa zote za Arsenal atawajibika kutoa ofa ya ununuzi wa Hisa zilizobaki na hilo litamfanya awe ndio Mmiliki pekee wa Klabu ya Arsenal.
Stan Kroenke ni Tajiri wa Kimarekani ambae vile vile ni Mmiliki wa Timu ya Mpira wa Vikapu, NBA, huko Marekani iitwayo Denver Nuggets.
Klabu za Manchester United na Liverpool zote zinamilikiwa na Matajiri wa Kimarekani ambao pia wanamiliki huko Marekani Klabu mbalimbali za Michezo.
Manchester United inamilikiwa na Familia ya Kimarekani ya kina Glazier na Liverpool inamilikiwa na Wamarekani wawili George Gillett na Tom Hicks.

No comments:

Powered By Blogger