Wednesday 17 March 2010

UEFA CHAMPIONS LIGI:
Leo Barca v Stuttgart na Bordeaux v Olympiakos!
• Droo ya Robo Fainali Ijumaa!!
• Chelsea nje, Drogba Nyekundu, Mourinho kidedea!!!
Leo usiku kuna mechi mbili zitakazotoa Timu 2 za mwisho kuungana na Arsenal, Manchester United, Lyon, Bayern Munich, Inter Milan na CSKA Moscow kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Barcelona ambao walitoka sare 1-1 na VfB Stuttgart katika mechi ya kwanza leo wako nyumbani Nou Camp na wanahitaji sare ya 0-0 au ushindi wowote ili watinge Robo Fainali.
Kwa Stuttgart, sare ya zaidi ya goli mbili ni ushindi kwao kwa sheria ya magoli ya ugenini.
Nao, Bordeaux, baada ya kushinda ugenini bao 1-0, leo wako nyumbani na wanahitaji sare tu ili Olympiakos na kusonga mbele.
Droo ya kupanga mechi za Robo Fainali itafanyika Ijumaa Machi 19.
Katika mechi za jana, Sevilla ilitunguliwa 2-1 wakiwa kwao na CSKA Moscow na hivyo CSKA kusonga mbele.
Mechi ya kwanza kwa Timu hizo ilikuwa ni sare ya 1-1.
Nako huko Stamford Bridge, Jose Mourinho alipokewa vizuri na Mashabiki wa Timu yake ya zamani Chelsea lakini bila shaka mwishoni walimlaani kwani Inter Milan waliifunga tena Chelsea na kuwabwaga nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Inter Milan ilishinda bao 1-0 kwa bao la Samuel Eto’o la dakika ya 79.
Na Nyota wa Chelsea Didier Drogba aliwashwa Kadi Nyekundu kwa mchezo mbaya na huenda UEFA ikamchukulia hatua kali zaidi kwani Drogba bado yuko kwenye uangalizi baada ya kutolewa kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI msimu uliokwisha kwa Kadi Nyekundu baada ya kumvaa Refa kwenye mechi ya Nusu Fainali na Barcelona na kufungiwa mechi 4 lakini akatumia kifungo cha mechi 2 na mbili kuwekwa kiporo kuchunga tabia yake.
Man United yakerwa na kutoadhibiwa Gerrard
Kwa mara ya pili ndani ya wiki moja Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard ameyakwepa marungu ya FA baada ya Marefa kumwokoa kwa kudai waliviona vitendo vyake kwenye mechi na hivyo hastahili kuadhibiwa tena.
Wiki iliyopita, kwenye mechi Liverpool aliyopigwa 1-0 na Wigan, Refa Andre Marriner alionekana kutukanwa na Gerrard na pia kuonyeshwa alama ya vidole ya V lakini Refa huyo alisema aliona vituko hivyo na kuvipuuza.
Juzi, kwenye ushindi wa Liverpool wa 4-1 dhidi ya Portsmouth, kamera zilimnasa Gerrard akimpiga kipepsi Mchezaji wa Portsmouth Michael Brown lakini Refa wa mechi hiyo Stuart Attwell amedai vitendo vya Gerrard havikustahili Kadi na hivyo FA haiwezi kuchukua hatua yeyote.
Jumapili Manchester United wanaikaribisha Liverpool Old Trafford kwenye mechi ya Ligi Kuu na endapo Gerrard angeshitakiwa na FA basi angeikosa mechi hiyo na Mahasimu wao wakubwa.
Manchester United haijazungumza kitu lakini taarifa zinadai wamekasirishwa na hatua ya FA ya kumtazama tu Gerrard mara mbili mfululizo wakati Mchezaji wao Rio Ferdinand alifungiwa mechi 3 na kuongezwa mechi moja zaidi alipokata rufaa kwa makosa kama ya Gerrard.
Hilo limewadhihirishia Manchester United kuwa wao hawatendewi haki na Marefa pamoja na FA.
Hii ni mara ya pili kwa Wachezaji wa Liverpool kutoadhibiwa kwa makosa ya wazi wakati Javier Mascherano alipoachiwa tu baada ya kuonekana wazi akimpiga Straika wa Leeds Jermaine Beckford mwezi Septemba mwaka jana kwenye mechi ya FA.

No comments:

Powered By Blogger