Thursday 16 September 2010

Allardyce amshukia Wenger!
• Adai anachota akili za Marefa waisaidie Arsenal
Sam Allardyce amemjia juu Arsene Wenger na kudai Meneja huyo wa Arsenal ni mwerevu na anatumia Vyombo vya Habari ili kuwarubuni Marefa na kuwafanya Wachezaji wake wasiguswe kwenye mechi.
Jumamosi, kwenye mechi ya Ligi Kuu, Abou Diaby wa Arsenal aliumia baada ya kugongana na Kipa wa Bolton, Adam Bogdan, na Wenger alidai kuwa Kipa huyo alikusudia na angepewa Kadi Nyekundu.
Wenger alitoa madai hayo kwenye program ya Arsenal ya kabla ya mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI dhidi ya Braga ya Ureno ambayo Washabiki huinunua kabla ya mechi.
Lakini Meneja wa zamani wa Bolton ambae sasa yupo Blackburn Rovers, Sam Allardyce maarufu kama Big Sam, ametamka: “Wenger ni Mtu mjanja! Anataka kuwarubuni na kuwachota akili Marefa ili Wachezaji wake wasiguswe kwenye mechi!
Wiki za nyuma Big Sam aliwahi kumpa vipande vyake Wenger pale alipotamka: “Hebu nimkumbushe Wenger. Timu yake ilikuwa ikuchukua Ubingwa na ndio ilikuwa Timu chafu kwa rafu kupita zote! Walikuwa Mabingwa huku wakiongoza kwa Kadi Nyekundu na Njano kupita Timu yeyote! Patrick Viera, Emmanuel Petit, Sol Campbell na Martin Keown walitumia kila mbinu chafu kushinda!”
Big Sam amesema hivi leo: “Wenger anatumia Vyombo vya Habari ili Marefa waisaidie. Ameleta dhana kuwa kila Timu inakusudia kuwaumiza Wachezaji wa Arsenal. Na nadhani Marefa wamechotwa akili na hilo na tunaona matokeo yake kwenye mechi!”
Allardyce aliongeza kwa kusema zile zama za Wachezaji kuingia Uwanjani ili kuwaumiza wenzao makusudi zimepitwa na wakati.

No comments:

Powered By Blogger