Tuesday 14 September 2010

Fergie: ‘Sijutii kumtema Rooney!’
• Pia, atafuta Nahodha mpya!
Licha ya kuiona na kukasirishwa na Manchester United kuutupa uongozi wa mabao 3-1 hadi dakika za majeruhi na kuruhusu Everton kusawazisha na kuifanya mechi ya Ligi Kuu Jumamosi kumalizika 3-3, Sir Alex Ferguson ameng’ang’ania kuwa uamuzi wake wa kumwacha Wayne Rooney ulikuwa ni sahihi.
Rooney hakucheza mechi ya Ligi Kuu ya Jumamosi dhidi ya Everton na Meneja wa Man United Sir Alex Ferguson alisema Mchezaji huyo aliachwa ili kumwepusha kuandamwa na Mashabiki wa Timu yake ya zamani Everton Uwanjani Goodison Park. Rooney amelipuliwa na baadhi ya Magazeti na kuhusishwa kutembea na changudoa wakati mkewe akiwa mja mzito.
Ferguson ametamka: “Sijutii. Sielezei zaidi. Sikutaka kuruhusu upuuzi wa kumshambulia na kumkebehi huko Goodison Park. Sina tatizo na yeye kucheza na Rangers.”
Ferguson alisistiza Rooney ni Mchezaji bora na hamna haja kwa ya kuelezea chochote kuhusu hilo.
Lakini Ferguson alitoa fununu kuwa yuko mbioni kumtafuta Nahodha wa kudumu wa Timu yake kwa vile Gary Neville amekuwa hachezi mfululizo kutokana na kuumia mara kwa mara.
Ikiwa Neville atacheza mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI na Rangers leo Jumanne Septemba 14 hiyo itakuwa mechi yake ya 600 kwa Man United lakini Ferguson amethibitisha hatavaa utepe wa Unahodha.
Jumamosi kwenye mechi na Everton licha ya Neville kucheza, Nahodha alikuwa Nemanja Vidic.
Ferguson ameelezea: "Gary bado ni Nahodha lakini natafuta mtu anaecheza kila wiki. Katika Miaka miwili mitatu iliyopita Gary amekuwa akiandamwa na majeruhi mfululizo. Mwenyewe Gary anajua kuwa kwa sasa hawezi kuchezeshwa kila mechi.”
Alipoulizwa ikiwa Ferdinand atapewa tena Unahodha endapo atacheza mechi na Rangers, Ferguson alijibu: “Sina la kusema. Wala sijafikiria hilo!”

No comments:

Powered By Blogger