Saturday, 18 September 2010

Spurs, WBA zazinduka Kipindi cha Pili na kushinda bao 3!
• Newcastle yairamba Everton ugenini!
Katika mechi za Ligi Kuu leo, Timu za Tottenham Hotspur na West Bromwich Albion, zikicheza nyumbani kila mmoja, zilijikuta ziko nyuma kwa bao 1-0 hadi mapumziko lakini zikazinduka Kipindi cha Pili na kushinda 3-1 kila mmoja wakati Spurs walipoikung’uta Wolves na WBA kuitwanga Birmingham.
Wolves walipata bao lao Kipindi cha kwanza mfungaji akiwa Steven Fletcher. Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 77 wakati Rafael van der Vaart aliposawazisha kwa penalti na dakika 3 kabla mpira kwisha Roman Pavlyuchenko alifunga la pili na kwenye dakika za majeruhi Beki Allan Hutton akapachika la 3.
West Bromwich walikuwa nyuma kwa bao moja hadi haftaimu lakini mabao ya Kipindi cha pili yaliyofungwa na Dann [alijifunga mwenyewe] dakika ya 51, Peter Odemwingie, dakika ya 59 na Olsson dakika ya 69 yaliwapa ushindi wa 3-1 dhidi ya Birmingham.
Nao Newcastle, wakiwa ugenini Goodison Park, walipewa ushindi na Mchezaji mpya kutoka Ufaransa, Hatem Ben Arfa baada ya shuti lake la Mita 25 la dakika ya 45 kwenda juu pembeni na kumpita Kipa wa Everton Tim Howard.
Huko Villa Park, Aston Villa walishindwa kumuaga kwa raha Meneja wa muda Kevin MacDonald anaeachia ngazi Jumatatu kumpisha Meneja mpya Gerrard Houllier anaeshika wadhifa, baada ya kuongoza kwa bao la frikiki ya Ashley Young, dakika ya 13, na kushindwa kulilinda na ndipo Bolton wakasawazisha kupitia Kevin Davies kwenye dakika ya 35.
Nako huko Ewood Park, Wenyeji Blackburn Rovers walitoka sare na Fulham ya 1-1 na kuwafanya Fulham wawe hawajafungwa katika mechi 5 zao za Ligi Kuu Msimu huu.
Blackburn walifunga mwanzo kwa kichwa cha Chris Samba kwenye dakika ya 36 na Fulham, ambao wako chini ya Meneja wa zamani wa Blackburn Mark Hughes, kusawazisha kwa kichwa cha Clint Dempsey kwenye dakika ya 56.

No comments:

Powered By Blogger