Saturday 18 September 2010

Stoke City 1 West Ham 1
Katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England leo, West Ham, wakicheza ugenini, wamepata pointi yao ya kwanza kwa Msimu huu baada ya kwenda sare 1-1 na Stoke City.
Scott Parker ndie alieifungia West Ham bao kwenye dakika ya 32 na bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Dakika 3 tu baada ya Kipindi cha Pili kuanza, Kenwyne Jones aliisawazishia Stoke City.
Matokeo hayo yameichimbia West Ham mkiani wakiwa na pointi moja katika mechi 5 wakati Stoke wapo nafasi ya 16 na wana pointi 4 kwa mechi 5.
BIGI MECHI: Man United v Liverpool
• Hodgson ahofia urafiki wake na Fergie!
Meneja wa Liverpool Roy Hodgson amekiri urafiki wake na Sir Alex Ferguson kesho utakuwa majaribuni wakati Manchester United itakapowakaribisha Watani zao wa Jadi Liverpool Uwanjani Old Trafford kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Hodgson amekuwa na urafiki wa muda mrefu na Ferguson lakini Meneja huyo wa Man United hakuwa na uhusiano mzuri na Meneja wa Liverpool aliepita, Rafael Benitez, ambae mara kadhaa alisimama mbele ya Wanahabari kumshambulia Ferguson.
Hodgson ametamka: “Ni rafiki yangu wa dhati. Lakini sijui yeye kama ananchukulia mimi kama rafiki wa dhati, hilo mwulizeni mwenyewe. Tunaongea vizuri tu na kutaniani.”
Hodgson akaongeza: “Siku moja nilimuuliza: ‘Sasa nimeingia Liverpool ina maana hatuongei tena?’ Hakukata simu ila hilo jibu alonipa!”
Hata hivyo, Hodgson, Miaka 62, amedai kuwa urafiki wao haujaathirika kwa yeye kutua Liverpool na ana uhakika atapewa glasi ya mvinyo wakikutana hiyo kesho huko Old Trafford.
Hodgson alimalizia kwa kusema: “Hamna urafiki wakati wa mechi. Lakini Washabiki hawaji uwanjani kuniangalia mimi au Fergie. Wao wanakuja kuwatazama Wachezaji 22. Lakini, Sir Alex ni Meneja bora katika historia ya Uingereza!”
Bifu la Pulis na Wenger laendelea!
Meneja wa Stoke City, Tony Pulis, amepeleka malamiko yake kwa Wasimamizi wa Ligi Kuu kumripoti Meneja wa Arsenal Arsene Wenger kwa kumshambulia Difenda wao Ryan Shawcross na kumwita ‘Mcheza Raga’.
Imeripotiwa kuwa Stoike City waliiandikia Arsenal barua mara mbili wakitaka kuombwa radhi lakini hawakupewa jibu lolote na sasa wameamua kupeleka malamiko kwa Ligi Kuu baada ya FA kutamka haitamchukulia hatua yeyote.
Mapema Mwaka huu, Ryan Shawcross alimvunja mguu Chipukizi wa Arsenal Aaron Ramsey na tangu wakati huo Wenger amekuwa akimwandama Mchezaji huyo kwa vijembe.

No comments:

Powered By Blogger