Monday 13 September 2010

Torres apondwa, Hodgson amtetea!
Kiungo wa zamani wa Liverpool, Jamie Redknapp, ambae sasa ni mtoa tathmini kwenye Kituo cha TV cha SKY wakati wa mechi za Ligi Kuu, amemponda Fowadi wa Liverpool, Fernando Torres, kwa kuwa chini ya kiwango na pia kutoonyesha ari yoyote katika mechi ya jana ya Ligi Kuu ambayo Liverpool ilitoka sare 0-0 na Birmingham Uwanjani Mtakatifu Andrew.
Torres amekuwa na wakati mgumu baada ya kuandamwa na maumivu ya nyonga na goti yaliyomfanya aukose Msimu uliopita kwa muda mrefu na pia kutong’ara kwenye Kombe la Dunia akiwa na Nchi yake Spain huko Afrika Kusini.
Jamie Redknapp amesema: “Kwa dakika 45, alikuwa ovyo. Alishindwa kumiliki mpira, alishindwa kufukuza mpira, akakata tamaa na angweza kupewa Kadi ya Njano kwa kucheza rafu.”
Lakini Meneja wa Liverpool, Roy Hodgson, amepinga na kutamka: “Sikubaliani na maoni ya Redknapp. Torres atarejea kiwango chake.”
Hodgson pia ameonyeshwa kushangazwa na baadhi ya wadau kutangaza Ubingwa kwa baadhi ya Timu huku Ligi ikiwa imechezwa mechi 4 tu.
Hadi sasa Liverpool wamecheza mechi 4 na wana pointi 5 wakiwa pointi 7 nyuma ya vinara Chelsea.

No comments:

Powered By Blogger