Saturday 9 August 2008

Real Wang’aka: Robinho hauzwi!
Kibao chawageukia!!!
Real Madrid baada ya kumwandama na kujaribu kumrubuni Ronaldo kwa muda mrefu sasa kibao kimewageukia wenyewe baada ya kujikuta wakiandamwa na Chelsea waliotoa ofa rasmi na ya hadharani ya kutaka kumnunua Robinho.
Imebidi Rais wa Real Ramon Calderon ajitetee vikali na kudai Robinho haondoki klabuni hapo ingawa Robinho mwenyewe anataka kuhama.
Siku ya Alhamisi Chelsea walitoa ofa ya kumnunua Robinho kwa Pauni milioni 19.7 na mwenyewe Robinho anataka sana kuungana na Meneja Mbrazil wa Chelsea Felipe Scolari.
Ramon Calderon alisisitiza: ‘Hamna njia Robinho ataondoka! Ni mchezaji wetu bora!’

MAN U KUSAINI MSHAMBULIAJI KABLA YA WIKI IJAYO!!!!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson ana matumaini ya kumsaini mshambuliaji mmoja kabla msimu mpya wa ligi haujaanza wiki ijayo.
"Tunaangalia njia tatu au nne hivi na tunategemea kufanikiwa," alisema Ferguson.
Mshambuliaji wa Tottenham Dimitar Berbatov inasemekana yuko kwenye listi hiyo ya wachezaji watatu au wanne wanaowaniwa. Wengine wanaotajwa ni Mchezaji wa Valencia David Villa, Klaas-Jan Huntelaar wa Ajax, Mshambuliaji wa Lyon Karim Benzema na wa Blackburn Roque Santa Cruz.
Kwa sasa Man U inakabiliwa na upungufu wa washambuliaji hasa ikizingatiwa Wayne Rooney mgonjwa ingawa Ijumaa alianza mazoezi, Ronaldo yuko nje kwa wiki 6 akiuguza enka aliyofanyiwa operesheni na hali ya Luis Saha kama kawaida ni ya kutotegemewa.
Juu ya Saha, Ferguson alitamka: ‘Kwanini ukate tamaa kuhusu Saha ati kwa sababu ameumia kidogo? Akiwa fiti ni hatari sana na anaweza kufunga zaidi ya magoli 20 kwa msimu. Kwa sasa yupo chini ya programu maalum na akifanikiwa hiyo tutakuwa na mchezaji fiti na wa kutumainiwa.’

No comments:

Powered By Blogger