Thursday, 7 August 2008


RONALDO ATAMKA: ‘NABAKI MAN U!’
Baada ya miezi kadhaa ya utata Cristiano Ronaldo jana usiku alithibitisha kwamba atabaki Manchester United.
Alisema: ‘Nathibitisha ntachezea Man U msimu ujao. Ntacheza kwa roho na moyo wangu wote na ntapigana na kulinda heshima ya jezi ya Man U nnayovaa kama nilivyokuwa nafanya siku zote. Kocha wangu Sir Alex Ferguson alifanya wema sana kuja kuniona mjini Lisbon siku chache zilizopita. Tulikuwa na mazungumzo ya wazi na ukweli kati ya watu wawili wanaopendana, wanaoheshimiana na wenye urafiki mkubwa. Sir Alex alinisikiliza na mimi nikamsikiliza na tukaona ni bora kwa pande zote nibaki Old Trafford. Kwa hilo sijitoi muhanga ila ni heshima kubwa. Kuna vitu muhimu vya kushinda nchini Uingereza. Nataka kutetea taji letu la Ulaya na kuisaidia Man U kuwa Mabingwa wa Dunia bila kusahau LIGI KUU na mashindano mengine. ’
Ronaldo akaongeza: ‘Sikutaka kuondoka Man U bila ridhaa yao na nitasema kitu ambacho sijamwambia mtu yeyote- laiti tusingechukua Ubingwa wa Ulaya nisingefikiria kuhama Man U. Lakini tulipochukua ubingwa huo, nilihisi miaka mitano nlokaa Man U nimesaidia kushinda kila kitu. Tulichukua LIGI KUU mara mbili na binafsi nimeshinda tuzo kadhaa ikiwa pamoja na Mfungaji Bora LIGI KUU na LIGI ya KLABU BINGWA ULAYA. Nilihisi nahitaji chalenji nyingine. Nilijua Real Madrid wananitaka na kwa muda nilitaka Man U wakubali ofa yao. Nilitaka kucheza Spain ili kuwa karibu na familia yangu. Lakini nataka hili liishe.’
Kwa unyenyekevu, Ronaldo akaongeza: ‘Nafahamu Klabu hii imenifanyia mengi. Daima ntashkuru. Walipokataa ofa ya Real ilionyesha dhahiri jinsi wanavyonithamini. Wakati ule sikuelewa hili vizuri lakini sasa nashkuru sana hilo lilitokea.’
Jana usiku Sir Alex Ferguson alizungumza: ‘Mashabiki lazima wafahamu ni vigumu sana kwa kijana mdogo kuvumilia wakati akirubuniwa na mihela kibao. Hasa kwa kijana alietoka Madeira [sehemu fukara huko Ureno nyumbani kwa Ronaldo]. Baba yake alikufa akiwa mdogo na jukumu la kuwatunza mama yake, dada na kaka yake liko kwake. Ronaldo siku zote ana furaha hapa. Haya yote sasa yamekwisha.’

No comments:

Powered By Blogger