Tuesday 14 October 2008

UEFA WAPIGA MARUFUKU UWANJA WA ATLETICO MADRID: Mechi ya Atletico Madrid na Liverpool kuchezwa kwingine!!

Chama cha Soka Ulaya, UEFA, kimeupiga marufuku Uwanja wa Klabu ya Atletico Madrid ya Spain uitwao Calderon Stadium kuchezewa mechi za UEFA CHAMPIONS LEAGUE kufuatia vurugu za mashabiki wa Klabu hiyo zilizoambatana na vitendo vya ubaguzi wa rangi kwenye mechi dhidi ya Marseille ya Ufaransa katika michuano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyochezwa tarehe 1 Oktoba ambayo Atletico Madrid walishinda 1-0.
Katika mechi hiyo Wachezaji wa Marseille ambao wengi ni weusi walipigiwa kelele za milio ya nyani na baada ya mechi basi lao lilishambuliwa. Vilevile Mashabiki wa Marseille waliokuwemo humo uwanjani walipigwa na hata Polisi waliingilia na kuwasulubu zaidi [tizama picha Mashabiki wa Marseille wakishambuliwa na Polisi].
Mbali ya Klabu ya Atletico Madrid kufungiwa uwanja wao vilevile wamekung'utwa faini nzito ya Euro 150,000 [takriban Sh milioni 225] na Meneja wao Javier Aguirre nae amepigwa marufuku asikae kwenye benchi la akiba, asiwepo kwenye vyumba vya Wachezaji kubadilishia nguo hapo uwanjani na pia asifanye mawasiliano yeyote na timu yake wakati wa mechi.
Adhabu hizi zinamaanisha mechi za Atletico Madrid na Liverpool hapo tarehe 22 Oktoba na ile na PSV Eindhoven ya tarehe 26 Novemba itabidi zichezwe kwenye uwanja mwingine ulio umbali usiopungua maili 200 toka jiji la Madrid.
Atletico Madrid wamepewa mpaka saa 7 mchana tarehe 17 Oktoba 2008 kukata rufaa kama hawakuridhika na adhabu.

No comments:

Powered By Blogger