LIGI KUU England: Mechi za Wikiendi hii na taarifa zake mbalimbali
Emmanuel Adebayor atakuwa kivutio kikubwa wakati Klabu yake ya zamani Arsenal itakapotua City of Manchester Stadium kucheza na Wenyeji Manchester City hapo kesho.
Adebayor, akiwa na Man City msimu huu, amefunga bao katika mechi zote 3 za Ligi Kuu walizocheza na kushinda zote.
Katika mechi hizo 3, ngome ya Man City haijaruhusu hata bao moja na inaongozwa na Mchezaji mwingine alietoka Arsenal, Kolo Toure.
Tottenham ni Klabu nyingine ambayo haijapoteza mechi msimu huu baada ya kushinda mechi zao zote 4 ikiwa na ile waliyoipiga Liverpool bao 2-1 siku ya ufunguzi wa mechi za Ligi Kuu lakini kesho wana mtihani mkubwa pale watakapowakaribisha Mabingwa watetezi Manchester United Uwanjani White Hart Lane.
Chelsea, ambao ndio vinara wa Ligi baada ya mechi 4 na kushinda zote, kesho wapo safarini hadi Uwanja wa Britannia kupambana na Stoke City.
Liverpool, ambao tayari katika mechi 4 wamepoteza mbili, watakwaana na Wababe wa Manchester United na Everton, Timu iliyopanda Daraja Burnley uwanjani Anfield. Hata hivyo, Burnley, wakicheza ugenini, hawajashinda wala kutoka droo na hawajafunga hata goli moja katika mechi zao mbili walizocheza huko ugenini.
Huko katikati ya England, mjini Birmingham, kutakuwa na kindumbwendumbwe cha Watoto wa mji mmoja kukutana na mechi hii, kwa sababu za usalama, itachezwa saa 6 mchana kwa saa za Uingereza na kuwakutanisha Birmingham City na Aston Villa Uwanjani St Andrews. Villa ndio wanaoonekana wenye nguvu baada ya kushinda mechi zote 4 zilizopita kati yao ukiwemo ushindi wa mabao 5-1 Uwanjani Villa Park mwaka jana.
Fulham wanawakaribisha Everton uwanjani Craven Cottage siku ya Jumapili huku Klabu zote zikitaka ushindi hasa baada ya kutoanza vizuri Ligi msimu huu. Fulham wameshinda mechi moja tu walipowafunga Portsmouth siku ya ufunguzi na wenzao Everton walifungwa mechi zao zote 2 za kwanza na kushinda ya 3 walipoiua Wigan.
Portsmouth hawana pointi hata moja hadi sasa baada ya mechi 4 na wawakaribisha Bolton ambao nao pia wanasuasua baada ya kupoteza mechi zao zote 3.
Blackburn Rovers , mpaka sasa wamecheza mechi 3 na kutoka droo moja na kufungwa mbili, wanawakaribisha Wolves uwanjani Ewood Park. Wolves wameanza msimu huu kwa kuwafunga Wigan, kutoka droo na Hull City na kufungwa na West Ham na Man City.
Sunderland, walioshinda mechi 2 na kufungwa 2, watakuwa nyumbani Stadium of Light kucheza na Hull City ambao wamecheza mechi 4 na kushinda moja, droo moja na kufungwa 2.
Wigan watakuwa wenyeji wa West Ham kwao DW Stadium msimu uliokwisha ilikuwa ikiitwa KC Stadium.
Wigan wameshacheza mechi 4, wameshinda moja na kufungwa 3 wakati West Ham wana mechi 3 na wameshinda moja, droo moja na kufungwa moja.
Ramos ni Kocha wa CSKA Moscow
Kocha wa zamani wa Tottenham na Real Madrid Juande Ramos ameteuliwa Meneja wa CSKA Moscow na kumbadili Mbrazil Zico.
Ramos, baada ya kutimuliwa Tottenham Oktoba, 2008, alipata kazi Real Madrid ya mkataba wa miezi 6 ulioisha mwishoni mwa msimu uliokwisha.
CSKA Moscow wako Kundi moja pamoja na Manchester United kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
No comments:
Post a Comment