Sunday 6 September 2009

NANI AMEFUZU KUSHUKA BONDENI?
-BRAZIL: Wamefanikiwa kuingia Fainali kutoka Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini leo alfajiri baada ya kuwafunga Mahasimu wao wakubwa Argentina waliokuwa kwao Rosario City kwa mabao 3-1.
Brazil ni Nchi pekee duniani kucheza Fainali zote za Kombe la Dunia.
Kocha wa Brazil Dunga amesema: “Ni furaha. Tumeifunga Timu ngumu yenye Mchezaji, Messi, ambae pengine kwa sasa ndie Bora kuliko wote! Tumewafunga Argentina kwao na wao hawajafungwa nyumbani kwenye michuano hii!”
-KOREA KASKAZINI: Hapo Juni 17, baada ya Iran kushindwa kuifunga Korea Kusini, Korea Kaskazini walihitaji suluhu tu na Saudi Arabia kwenye mechi iliyochezwa Riyadh siku hiyo hiyo.
Korea Kaskazini walipata suluhu ya 0-0 na kutinga Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipofikia Robo Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1966 iliyochezwa Uingereza na kutolewa na Portugal, ikiwa na Mchezaji hatari wakati huo, Eusebio, kwa mabao 5-3 ingawa walikuwa wakiongoza 3-0 hadi mapumziko.
-UHOLANZI: Juni 6, Uholanzi ilimudu kuwa Nchi ya kwanza kutoka Ulaya kutinga Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuwafunga Iceland ugenini mabao 2-1 na mpaka hapo walikuwa wameshinda mechi zao zote kwenye Kundi lao.
-KOREA KUSINI: Kwa kuweza kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani, Korea Kusini sasa wametimiza kucheza Fainali yao ya 7 mfululizo. Waliingia Fainali Juni 6 walipowafunga Falme ya Nchi za Kiarabu mabao 2-0 mjini Dubai.
-AUSTRALIA: Australia walipata ubwete kutinga Fainali za Kombe la Dunia waliposhinda mechi zao zote 6 bila kufungwa hata goli na waliupata uhakika huo baada ya kutoka suluhu 0-0 na Qatar mjini Doha hapo Juni 6, 2009.
-JAPAN: Japan ilikuwa Nchi ya kwanza kupata tiketi ya kwenda Afrika Kusini walipoifunga Uzbekistan kwao mjini Tashkent bao 1-0. Hiyo pia ilikuwa Juni 6.

No comments:

Powered By Blogger