Tuesday 8 September 2009

Rafa awaonya Mawinga wake Babel na Riera
Ryan Babel alitoka hadharani hivi karibuni na kusema bora aende kucheza kwao Uholanzi Timu ya Ajax ili ajihakikishie kuchukuliwa Timu ya Taifa ya Uholanzi ili acheze Fainali za Kombe la Dunia kwa sababu akiwa Liverpool hana namba ya kudumu na hilo limemfanya asichukuliwe Timu ya Uholanzi katika mechi za hivi karibuni.
Babel hakutajwa kwenye Kikosi cha Uholanzi kilichochaguliwa kucheza mechi za Kombe la Dunia Jumatano iliyopita ila aliitwa baadae baada ya Mshambuliaji mmoja kuumia.
Inaelekea kauli ya Babel imemtibua Kocha Rafa Benitez ambae alitoka na kudai kuwa Babel na Riera wote wanalilia kucheza na wote wanacheza pozisheni moja hivyo kuna ushindani mkubwa.
Benitez anasema: “Ujumbe ni rahisi tu. Kiwanjani kila Mchezaji lazima adhihirishe ana uwezo. Babel anajua hawezi kuhama kwa sasa. Ni lazima afanye kazi turidhike. Ni Mchezaji mzuri na ana kipaji. Ni muhimu tuongee nae na tuone anapata maendeleo gani.”
Sasa balaa la Wafaransa lawakumba Man City kwa kumpora Chipukizi!
Klabu ya Ufaransa Rennes imethibitisha kuwa wameishitaki Manchester City kwa FIFA kwa kumpora Chipukizi Jeremy Helan mwanzoni mwa mwaka huu.
Mwaka 2008, Kijana huyo Helan, miaka 17, alitakiwa na Manchester United lakini Rennes wakagoma kumtoa na ndipo Man City wakajikita na kumchukua ingawa Rennes walidai wana mkataba na Helan kuwa atasaini mkataba mwingine kama Mchezaji wa Kulipwa akifikisha miaka 17.
Huko Ufaransa hairuhsiwi mtoto chini ya miaka 18 kusaini mkataba wa kuwa Mchezaji wa Kulipwa wakati England wanaruhusiwa wakifikisha miaka 17.
Hivi juzi tu FIFA imeifungia Chelsea hadi 2011 kutosajili Mchezaji baada ya kupatikana na hatia ya kumpora Chipukizi Gael Kakuta kutoka FC Lens ya Ufaransa.
Siku mbili baadae ikaibuka Klabu nyingine ya Ufaransa Le Havre na kudai Manchester United imewapora Kijana wao Pogba kwa kuwarubuni Wazazi wake na kuwapa fedha taslimu na nyumba.
Hata hivyo, ingawa Le Havre imedai imepeleka mashtaka FIFA, FIFA imesema haijapokea chochote na wakati huo huo Manchester United imewataka Le Havre waache madai hayo au la watawashitaki.
Ingawa Rennes imepeleka kesi FIFA na wao pia wamepelekwa Mahakamani na upande wa Chipukizi Helan wakivutana kuhusu nini kilisainiwa wakati Helan alipojiunga na Rennes.

No comments:

Powered By Blogger