Thursday 10 September 2009

Sir Alex Ferguson aitetea Man U!
Sir Alex Ferguson ameutetea msimamo wa Klabu yake Manchester United kuhusu kuwasaini Vijana Wadogo toka nje ya Uingereza na kudai wao wanaburuzwa kwenye mgogoro huo kwa sababu wao ni klabu kubwa.
Kufuatia kufungiwa kwa Chelsea na FIFA kutosajili Wachezaji hadi 2011 baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka taratibu walipomsaini Chipukizi Gael Kakuta kutoka FC Lens ya Ufaransa, Manchester United nao wakajikuta wakituhumiwa na Klabu nyingine ya Ufaransa Le Havre kuhusu kumsajili Bwana Mdogo Pogba.
Wakati huo huo Klabu ya Italia Fiorentina imewasiliana na FIFA kuhusu Man U kumchukua Kijana Michele Fornasier na kudai imempora ingawa Man U imesema Fiorentina haina mkataba na kijana huyo.
Ferguson amesema: “Siku zote watatuingiza kwenye migogoro kwa sababu tu ni Man U! Sasa kumekuwa na mtindo wa kurukia treni bila kujua iendako!”
Ferguson amesisitiza Man U haiwezi kutoa pesa kwa Wazazi wa Wachezaji kama inavyodaiwa na amesema itabidi Le Havre wajibu kwa nini walitoa tuhuma hizo zisizo msingi.
Ferguson akaongeza: “Tuhuma hizi zimeletwa na Mkurugenzi mmoja wa Le Havre mwenye kinyongo na sasa itabidi afute usemi huo! Sisi tunasajili kisheria. Klabu nyingine hufanya mambo kichinichini lakini sisi tunajiamini ni wakweli!”
Argentina wako njia panda kwenda Bondeni!
Argentina wako hatarini kukosa kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1970 baada ya kufungwa na Paraguay 1-0 leo alfajiri.
Kikosi cha Diego Maradona wapo nafasi ya 5 wakiwa pointi moja nyuma ya Ecuador huku kumesalia mechi 2 kwa kila timu na ni Timu 4 za juu ndizo zinazoingia moja kwa moja Fainali huku ya 5 ikicheza na Mshindi wa 4 toka Kundi la Nchi za Marekani ya Kati, Kaskazini na Caribean.
Wakati Argentina wanaweweseka, Brazil, inayoongoza Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini, ikichezesha Kikosi ‘dhaifu’ bila ya Kaka, Lucio na Fabiano waliokuwa na Kadi na pia Robinho aliekuwa majeruhi, waliifunga Chile 4-2 huku Mshambuliaji Nilmar akifunga bao 3 mguuni kwake na moja kufungwa na Baptista.
Ingawa Chile walifungwa bado wako nafasi ya 3.
Katika mechi nyingine, Ecuador waliifunga Bolivia 3-1 kwa magoli ya Edison Mendez, Antonio Valencia [wa Man U] na Cristian Benitez [Birmingham].
Uruguay wamejipa pia matumaini baada ya ushindi wa 3-1 juu ya Colombia na Venezuela wakaichabanga Peru 3-1.
Kipigo cha Argentina ni cha 4 katika mechi 5 za mwisho walizocheza kwenye Kundi lao hilo na presha inazidi kumbana Maradona.
Lakini mwenyewe Diego Maradona ametamka: “Mpaka tone langu la mwisho la damu, ntapigana kuifanya Argentina iingie Fainali! Hatupo nje ya Kombe la Dunia! Siogopi kusakamwa na siogopi mtu! Ntaendelea bila kujali nani ananiponda!”
Mechi zilizobaki za Argentina ni dhidi ya Peru na Uruguay.
Msimamo wa KUNDI hilo ni:
-Brazil pointi 33
-Paraguay pointi 30
-Chile pointi 27
-Ecuador pointi 23
-Argentina pointi 22
-Uruguay pointi 21
-Venezuela pointi 21
-Colombia pointi 20
-Bolivia pointi 12
-Peru pointi 10
MATOKEO KOMBE LA DUNIA: MAREKANI YA KUSINI
Jumatano, 9 Septemba 2009
Bolivia 1 v Ecuador 3
Uruguay 3 v Colombia 1
Paraguay 1 v Argentina 0
Venezuela 3 v Peru 1
Brazil 4 v Chile 2

MATOKEO KOMBE LA DUNIA: AFRIKA
Jumatano 9 Septemba 2009
Cameroun 2 Gabon 1
Magoli Cameroun Wafungaji Jean Makoun, dakika ya 25 na Samuel Etoo dakika ya 64.
Goli la Gabon Mfungaji Daniel cousin dakika ya 90.

No comments:

Powered By Blogger