Tuesday 8 September 2009

MAN U WAIONYA LE HAVRE!
Manchester United imeionya Klabu ya Le Havre ya Ufaransa kuwa watachukua hatua za kisheria ikiwa Klabu hiyo haitaacha kutoa madai kwamba waliwapa pesa Wazazi wa Chipukizi Paul Pogba, miaka 16, ili kijana huyo asaini kwao.
Rais wa Le Havre, Jean-Pierre Louvel, amedai kuwa Manchester United iliwapa Wazazi wa Pogba, Baba na Mama, Pauni 87,000 kila mmoja pamoja na nyumba ya kuishi mjini Manchester.
Louvel aliendelea na madai yake kwa kusema kuwa wameshapeleka malalimiko yao FIFA.
Wiki iliyopita, FIFA iliifungia Chelsea hadi mwaka 2011 kutosajili Mchezaji yeyote baada ya kupatikana na hatia ya kumchukua Mchezaji chipukizi Gael Kakuta kutoka FC Lenz ya Ufaransa kinyume cha taratibu.
Manchester United imesema imefuata taratibu zote za UEFA na FIFA na kwamba uhamisho huo ikiwa pamoja na Mikataba yake, ilipitiwa na kupasishwa na FA, Chama cha Soka England, pamoja na uongozi wa Ligi Kuu England. Vilevile, Man U walisisitiza kuwa kufuatana na kanuni za Klabu yao pamoja na sheria za soka wao hawawezi kutoa fedha au kuwanunulia nyumba Wzazi wa Mchezaji.
Hata hivyo, inasemekana Chama cha Soka cha Ufaransa, kufuatia shinikizo la Le Havre, bado hakijatoa Cheti cha Kimataifa cha Uhamisho na ndio maana FIFA hawajaubariki uhamisho huo.
Maradona aandamwa baada ya Brazil kuwachoma mkuki moyoni!!!
*Wengi waponda mbinu zake kwenye kipigo cha 3-1 na Brazil!
Tangu walipokuwa Wachezaji, Dunga na Maradona, walikuwa dunia tofauti. Dunga alikuwa mpiganaji anaehaha uwanja mzima akitafuta ushindi kwa kila hali wakati Diego Maradona alikuwa ni Mshambuliaji alieamini mashambulizi ya ufundi wa hali ya juu ndio njia bora.
Lakini, Jumamosi iliyopita, Argentina ya Maradona, iliyoahidi kushambulia mechi yote, ilijikuta ikibamizwa na Brazil iliyosimama ngangari kwa bao 3-1 na kufanya mategemeo ya Argentina kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini kuwa kwenye hatihati huku wakiwa wamebakiwa na mechi 3 tu.
Ingawa falsafa ya Dunga kuhusu uchezaji wa Brazil haumpi Mashabiki wengi kwani Kikosi chake si ile Brazil inayocheza ‘soka tamu’ kama la enzi za kina Pele, Bebeto, Romario, Zico na hata Ronaldo, lakini ni Brazil ya Dunga ndiyo iliyobeba Copa America na Kombe la Mabara hivi juzi na sasa kutinga Fainali Kombe la Dunia huku wana mechi 3 mkononi!
Juu ya yote, ni Brazil ya Dunga iliyomudu kuwapiga mahasimu wao wakubwa Argentina mara 3 tangu mwaka 2006!
Bila shaka Maradona, muumini wa mashambulizi mfululizo, atakerwa sana na timu yake jinsi ilivyoshindwa kuleta hatari golini mwa Brazil na, bila shaka pia, udhaifu wa Argentina kwenye ngome utampa Maradona kero kubwa zaidi kwani, kwenye kipindi cha kwanza walipachikwa na Brazil bao 2 zote zikitokana na frikiki za Elano walizoshindwa kuzilinda na badala yake, kwa goli la kwanza, kumwacha Luisao akipiga kichwa akiwa pekee bila kuwepo ulinzi wowote na bao la pili lilifungwa tena kwa frikiki waliyoshindwa kujihami nayo vizuri na mpira kumfikia Fabiano aliefunga kilaini.
Magazeti ya huko Argentina, baada ya mechi hiyo, yameweka vichwa vya habari vikubwa wakiiponda Timu ya Maradona na kuiita sio timu huku mengine yakidai Maradona ameshindwa kuibadili Argentina.
Fadhaa ya wengi Argentina inaangukia kwa Mchezaji wao Bora ambae wengi wanaamini kuwa ndie bora kuliko wote kwa sasa duniani , Lionel Messi, ambae anang’ara sana akiwa na Klabu yake FC Barcelona lakini akiwa na jezi ya Argentina hupwaya sana na siku ya mechi na Brazil alijikuta yuko mpweke sana katikati ya ngome imara ya Brazil.
Nalo Gazeti moja huko Argentina, mbali ya kumponda Maradona, pia lilimcharukia Messi na kunyooshea kidole maamuzi yake mabovu uwanjani na uchoyo wa kutoa pasi kwa wenzake.
Argentina wako nafasi ya 4 ambayo ndiyo nafasi ya mwisho kwa Timu kufuzu kuingia Fainali za Kombe la Dunia moja kwa moja na Timu iliyo nafasi ya 5 itabidi icheze na Timu itayomaliza nafasi ya 4 toka Kundi la Nchi za Marekani ya Kati, Kaskazini na Caribean ili kupata timu moja kwenda Fainali.
Lakini, nyuma tu ya Argentina, wakiwa pointi mbili nyuma, ni Ecuador na Colombia na wote bado wapo kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo ya 4 na ya 5.
Hivyo njia kwa Argentina si nyeupe kwani Jumatano wanakwenda ugenini kucheza na timu ngumu ya Paraguay walio nafasi ya pili nyuma ya Brazil.
Kisha mwezi Oktoba watacheza na Peru nyumbani na kumaliza ugenini na Uruguay.

No comments:

Powered By Blogger