Thursday, 30 July 2009

Alonso aomba rasmi uhamisho!
Kiungo wa Liverpool Xabi Alonso, miaka 27, hatimae amewasilisha maombi rasmi ya kutaka kuhama Klabu yake na kwenda Real Madrid.
Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Spain ameng’ang’ania kuhama baada ya kuudhiwa na kitendo cha Liverpool kutaka kumuuza msimu uliokwisha ili wamchukue Gareth Barry wa Aston Villa wakati huo.
Barry hivi majuzi amehamia Manchester City.
Ingawa Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, amekuwa akisema Alonso hauzwi inaaminika kuhama kwa Alonso kupo ikiwa tu Klabu hizo mbili zitaafikiana dau lake huku Liverpool wakitaka Pauni Milioni 30 na Real wako tayari kutoa Pauni Milioni 25.
Taarifa hizi zimeendelea kudai kuwa kwa sababu sasa Alonso ameshatoa msimamo wake kimaandishi basi Liverpool watalazimika kumuuza.
Alonso alinunuliwa na Liverpool mwaka 2004 na kwa Pauni Milioni 10.5.
Wenger haingii sokoni licha ya kuwauza Ade na Kolo!!!
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ametoboa kuwa hatoenda sokoni kwa kiwewe cha kuwakosa Adebayor na Kolo Toure ambao wamenunuliwa na Manchester City.
Kuna baadhi ya Wadau wa Soka wa Arsenal wamemlaumu sana Wenger kwa kuruhusu kuuzwa kwa Wachezaji hao ambao Wadau hao wanaamini ni nguzo kubwa kwa Klabu hiyo.
Mpaka sasa Wenger amenunua Mchezaji mmoja ambae ni Mlinzi Thomas Vermaelen kutoka Ajax.
Hata hivyo kuna habari ambazo zimeanza kuota mizizi kuwa Nahodha wao wa zamani Patrick Viera anataka kurudi Arsenal akitoka Inter Milan.
Elano ahamia Galatasaray
Galatasaray ya Uturuki imekamilisha taratibu za kumchukua Kiungo wa Brazil, Elano, miaka 28, anaecheza Manchester City kwa mkataba wa miaka minne.
Elano alisainiwa na Man City mwaka 2007 kwa dau la Pauni Milioni 8 kutoka Klabu ya Ukraine Shakhtar Donetsk na ameichezea Man City mechi 80 na kufunga mabao 18.
Mpaka sasa Man City ishawachukua Washambuliaji Roque Santa Cruz, Carlos Tevez na Emmanuel Adebayor, Kiungo Gareth Barry na Mlinzi Kolo Toure.
Jitihada zao za kuwabeba Walinzi John Terry kutoka Chelsea na Joleon Lescott kutoka Everton mpaka sasa zimepiga mwamba baada ya Klabu zao kugoma kumuuza.

No comments:

Powered By Blogger