Wednesday 29 July 2009

Kolo Toure aafikiana na Man City!
Kolo Toure amefikia makubaliano na Klabu ya Manchester City kuhusu maslahi yake na sasa atapimwa afya ili kukamilisha uhamisho wake kutoka Arsenal kwa dau linaloaminika ni zaidi ya Pauni Milioni 15.
Toure amekuwa akiichezea Arsenal tangu mwaka 2002 wakati Arsene Wenger alipomtoa kwao Ivory Coast kwa dau dogo sana.
Inaaminika Toure amesaini mkataba wa miaka minne na yeye atakuwa Mchezaji wa pili wa Arsenal kuhamia Man City baada ya Emmanuel Adebayor kuhamia huko hivi karibuni.
Liverpool wathibitisha Arbeloa kauzwa Real!!!
Liverpool imetoa uthibitisho kwamba wamefikia makubaliano na Real Madrid ili Beki wao Alvaro Arbeloa ahamie Real Madrid.
Uhamisho huo utaigharimu Real Pauni Milioni 3 na nusu na inasemekana Arbeloa atasaini mkataba wa miaka mitano.
Arbeloa alianza uchezaji wake wa soka Real Madrid na kisha kuhamia Deportivo La Coruna na baadae Liverpool.
KOMBE LA ASIA: Tottenham waitungua West Ham na kutinga Fainali! Hull City watinga Fainali kwa matuta!!
Wakicheza vizuri sana, leo huko Beijing, Uchina, Tottenham wamewatundika wenzao wa Ligi Kuu England West Ham bao 1-0 bao lililofungwa na Jermain Defoe dakika ya 75.
Mechi hiyo iliingia dosari baada ya Mchezaji wa West Ham Luis Boa Morte kuumia goti na taarifa zimesema huenda akawa nje ya Uwanja kwa muda mrefu.
Katika mechi iliyofuata, Hull City walitoka sare na wenyeji wao Beijing Guoan bao 1-1 na ndipo zikapigwa penalti tano na ngoma ikawa tena droo baada ya kila Timu kukosa moja.
Lakini Hull City wakaibuka kidedea baada ya kufunga penalti yao ya 6 na Beijing Guoan kupaisha ya kwao.
Sasa Fainali ni kati ya Tottenham na Hull City.
Kurudi Hargreaves uwanjani kuna utata!!!
Kiungo wa Manchester United Owen Hargreaves ambae yuko nje ya uwanja tangu mwaka jana Septemba kwa matatizo ya magoti yake yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji kila goti lake huko Marekani huenda akalazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda zaidi baada ya kuambiwa na Madaktari bado inabidi aendele na tiba huko huko Marekani.
Akiongea huko Ujerumani ambako Manchester United leo wanapambana na Boca Juniors ya Argentina katika mashindano ya Audi Cup, Sir Alex Ferguson amesema: ‘Tulitegemea atakuja hapa Ujerumani kuungana na sisi lakini imeonekana bora aendelee na matibabu zaidi huko Marekani.’

No comments:

Powered By Blogger