Sunday 26 July 2009

Ferguson: ‘Man City ni Klabu Ndogo!’
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amesema Manchester City ni ‘Klabu ndogo yenye falsafa finyu!’
Kauli hiyo ya Ferguson imefuatia kutundikwa bango kubwa sana katikati ya Jiji la Manchester la rangi ya kibluu, ambayo ndiyo rangi ya Man City, likiwa na picha ya Carlos Tevez na maandishi: ‘Carlos Tevez, karibu Manchester.’
Alipoulizwa, Ferguson nae akahoji: ‘Ni Man City sio? Wao ni Klabu ndogo yenye falsafa finyu! Siku zote hawana la kuongea ila Manchester United! Wanadhani kumchukua Tevez ni ushindi! Ni upuuzi tu!’
Hivi karibuni, Man City wametumia pesa nyingi sana kuwanunua Emmanuel Adebayor kutoka Arsenal kwa Pauni Milioni 25, Gareth Barry kutoka Aston Villa Pauni Milioni 12, Roque Santa Cruz kutoka Blackburn Pauni Milioni 18 na Tevez kwa Pauni Milioni 25.
Ferguson, akiwa China kwenye ziara ya Asia pamoja na Timu yake, pia alidai Adebayor alijaribu ‘kujiuza’ Man U kabla ya kukamilisha usajili Man City.
Ferguson amesema: ‘Mtu akikupa kitita kama cha Man City ni vigumu kukataa! Ndio maana Wachezaji wanaenda huko. Katika dakika za mwisho kabla Adebayor hajasaini Man City, yeye au Wakala wake, walitupigia simu na waliwapigia simu Chelsea! Adebayor alikuwa akihaha kuhamia kwetu au Chelsea!’
Hatimaye Liverpool wapata ushindi wa kwanza mechi za kirafiki!
Leo, Liverpool hatimaye wamepata ushindi wao wa kwanza katika mechi za kirafiki za matayarisho kwa ajili ya msimu mpya waliposhinda huko Singapore kwa kuifunga Timu ya Taifa ya Singapore bao 5-0.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Kijana kutoka Hungary, Krisztian Nemeth, bao 2, Andriy Voronin, Allbert Riera na Fernando Torres.
Kombe la Wembley: Leo Barcelona 4 El Ahly 1, Tottenham v Celtic kucheza baadae leo!
Katika mashindano ya kugombea Kombe la Wembley yanayochezwa mjini London Uwanjani Wembley, El Ahly ya Misri, leo imepata kipigo cha pili, cha kwanza kikiwa 5-0 walichokung’utwa na Celtic ya Scotland siku ya Ijumaa, na leo Barcelona wakawapiga 4-1.
Mechi nyingine ya Kombe hilo ilichezwa Ijumaa wakati Tottenham na Barcelona kutoka suluhu 1-1.
Leo, saa 12 saa za bongo, Tottenham watakumbana na Celtic.
Portsmouth wathibitisha Crouch kwenda Tottenham
Meneja wa Portsmouth, Paul Hart, amethibitisha kuwa Mshambuliaji ‘ngongoti’, Peter Crouch, miaka 28,atanunuliwa na Tottenham Hotspurs baada ya Klabu hizo mbili kufikia makubaliano yanayosadikiwa kuwa ni ada ya Pauni Milioni 10.
Crouch, ambae alianzia kuichezea Tottenham siku za nyuma, amecheza na Portsmouth msimu mmoja tu toka ahamie hapo kutoka Liverpool.
Hangzhou Greentown 2 Man U 8
Manchester United leo wamemaliza ziara yao ya Asia kwa kishindo pale walipopata ushindi wa kishindo baada ya kuwakung’uta wenyeji wao Hangzhou Greentown mabao 8-2.
Mpaka mapumziko, Man U walikuwa mbele mabao 4-0, wafungaji wakiwa Michael Owen, bao 2, Berbatov na Zoran Tosic bao 1 kila mmoja. Kipindi cha pili Ryan Giggs akafunga 3 na Nani akafunga bao
1.

No comments:

Powered By Blogger