Saturday 25 July 2009

Mchezaji umri mdogo katika historia!!!!
Julio Cesar Baldiviesco, baba wa Kijana anaeaminika kuwa ndio Mchezaji wa Kulipwa wa Soka ambae ni mdogo kupita wote katika historia, amelazimika kujitoa kama Kocha wa Klabu ya Nchini Bolivia Aurora baada ya Menejimenti kumwambia asmchezesha mwanawe huyo aitwae Mauricio [pichani] aliecheza Jumapili iliyokwisha akiwa na umri wa miaka 12 na kuweka hiyo rekodi ya Dunia.
Baldiviesco alimwingiza Mwanawe kutoka benchi zikiwa zimebaki dakika 9 huku Aurora ikiwa nyuma bao 1-0 ikicheza na La Paz na uamuzi huo umezua mgogoro mkubwa huko Bolivia huku baadhi wakitaka kuwa na umri wa chini wa kuruhusu Wachezaji wa Kulipwa.
Baldiviesco, alieichezea Bolivia Kombe la Dunia mwaka 1994 huko Marekani, ametamka: ‘Inasikitisha kwa watu kutokukubali vipaji! Nchi hii na Dunia lazima ijue Bolivia kuna vipaji lakini Bolivia vipaji hukatwa miguu!’
Beckham apigwa faini!
David Beckham amepigwa faini ya Dola 1,000 na MLS [Major League Soccer], Chama cha Soka Marekani, baada ya kufarakana na Mshabiki mmoja wakati Timu yake LA Galaxy ilipokuwa ikicheza mechi ya kirafiki na AC Milan wiki iliyokwisha.
Katika mechi hiyo kuna kikundi cha Mashabiki kilichokuwa kikizomea na kumkashifu Beckham kwa vile aliiacha LA Galaxy na kwenda kucheza AC Milan kwa mkopo ili kujipa nafasi ya kuchukuliwa Timu ya Taifa ya England kitu ambacho alifanikiwa kukifanya na sasa ndie Mchezaji aliecheza mechi nyingi England kwa kucheza jumla ya mechi 112.
Sunderland yambeba Nahodha wa Marseille!
Klabu ya Sunderland imemnunua Kiungo na Nahodha wa Marseille ya Ufaransa, Lorik Cana, miaka 25, ambae ni raia wa Albania, kwa mkataba wa miaka minne.
Cana alijiunga Marseille akitokea Paris St Germain mwaka 2005 na ameshaichezea Timu ya Taifa ya Albania mara 31.
Bolton wachukua wawili kwa mpigo!!
Meneja wa Bolton, Gary Megson, amefanya usajili wake wa nne kwa msimu ujao baada ya kuwachukua Zat Knight kutoka Aston Villa na Sam Ricketts kutoka Hull City kwa madau ambayo hayakutajwa ila wote wawili wamepewa mkataba wa miaka mitatu kila mmoja.
Awali Megson aliwanunua Sean Davis kutoka Portsmouth na Paul Robinson kutoka West Bromwich Albion.

No comments:

Powered By Blogger