Sunday 19 July 2009

Man City yafungwa Bondeni!!
Manchester City wakiwa kwenye ziara ya mechi 3 huko Afrika Kusini wameanza ziara hiyo kwa kufungwa mechi ya kwanza na Orlando Pirates bao 2-0 kwenye mechi iliyochezwa Polokwane.
Mabao ya Orlando Pirates yalifungwa na Lucas Thwala kwa penalti na la pili na Phenyo Mongala.
Siku ya Jumanne Man City watacheza na Kaizer Chiefs mjini Durban na kumaliza ziara hiyo kwa kucheza Jumamosi mjini Pretoria.
Oliveira anunuliwa Abu Dhabi na kuweka rekodi!!!
Mchezaji wa Kimataifa wa Brazil Ricardo Oliveira, miaka 29, [pichani] aliekuwa akicheza Spain kwenye Klabu ya Real Betis amenunuliwa na Klabu ya Abu Dhabi Al-Jazira kwa dau la Pauni Milioni 19 ambayo ni rekodi kwa ununuzi wa Mchezaji huko Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.
Klabu ya AL-Jazira inamilikiwa na Sheikh Mansur Ben Zayed al-Nahyan, mmoja wa Wanafamilia kutoka Koo ya Kifalme ya huko Abu Dhabi, ambae pia ni Mmiliki wa Manchester City.
Oliveira mwenyewe, ambae amechezea Timu ya Taifa ya Brazil mara 11, ameungama kuwa anajua Ligi ya Falme za Nchi za Kiarabu, iliyoanzishwa rasmi mwaka jana, kiwango chake ni duni ukilinganisha na Spain, lakini ofa aliyopewa imemfanya yeye na Familia yake washindwe kuikataa.
Bayern Munich watishia kuishitaki Real Madrid!!
Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge ametishia kuchukuwa hatua dhidi ya Real Madrid kama wataendelea kumrubuni Mchezaji wao Franck Ribery.
Kiungo huyo kutoka Ufaransa ameshaambiwa na Mabosi wa Bayern kuwa hauzwi msimu huu lakini Vigogo hao wa Spain wameendelea kumfuata na kusababisha hasira za Bayern Munich.
Rummenigge amekaripia: ‘Real wamekuwa wakivunja kanuni za FIFA wiki nenda rudi kwa sababu hawajapata kibali chetu kuongea na Ribery au Wakala wake. Nitawasiliana na Perez [Rais wa Real] kumtaka aache upuuzi huu au tutawaripoti FIFA.’

No comments:

Powered By Blogger