Wednesday, 22 July 2009

Mascherano ana nia kwenda Spain!!
Kiungo wa Liverpool anaetoka Argentina, Javier Mascherano, ana nia ya kweli kuhamia Spain kwa sababu amechoshwa na maisha ya Uingereza.
Inasadikiwa Mascherano angependa kuhamia Real Madrid au Barcelona na habari hizi zimethibitishwa na Wakala wa Mchezaji huyo, Walter Tamer, ambae amesema: ‘Barcelona ni rahisi kwake kwenda kwani angependa kuishi Spain. Amechoka na England. Hata mkewe hajapewa visa ya kudumu ya kuishi Uingereza. Liverpool hawataki kumuuza lakini wakipewa ofa nzuri wataongea tu!’
Hili ni pigo kwa Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, kwani Kiungo wake mwingine wa kutumainiwa, Xabi Alonso, nae pia anataka kutimkia Real Madrid.
Eriksson arudi tena England, yuko Notts County!!
Meneja wa zamani wa England, Sven Goran Eriksson, amateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Soka kwa mkataba wa miaka mitano na Klabu iliyo League Two, Notts County, na ameahidi kuipandisha hadi Ligi Kuu.
Eriksson baada ya kuondoka kama Meneja wa England aliifundisha Manchester City kwa msimu mmoja tu kisha akaondolewa na akapata kazi ya kuifundisha Timu ya Taifa ya Mexico ambako hakudumu nayo muda mrefu.
Mwenyewe Eriksson amesema hakwenda Notts County kutafuta pesa bali ni kwa sababu moja tu na nayo ni changamoto ya kuipandisha Ligi Kuu.
Wenger asema Nasri atakuwa nje wiki 6 tu!!
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ana matumaini Samir Nasri atarudi uwanjani baada ya wiki 6 na sio miezi mitatu iliyotangazwa mara baada ya kuvunjwa mguu huko kambini Austria hapo jana.
Wenger amesema: ‘Alimpora mtu mpira aliekuwa akitaka kuupiga na ndipo alipovunjwa mguu! Lakini ingawa amevunjika lakini si vibaya kama tulivyoogopa! Tunategemea atarudi baada ya wiki 6. Lakini tunae Rosicky ameshapona na Eduardo atarudi baada ya miezi miwili.”
Drogba asaini mkataba mpya Chelsea!
Mshambuliaji wa Chelsea Didier Drogba, umri miaka 31, anategemewa kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu kufuatana na kauli ya Meneja wake Carlo Ancelotti.
Drogba, ambae jana alifunga bao moja na Lampard la pili pale Chelsea walipowafunga Inter Milan kwenye mechi ya kirafiki, ameshaifungia Chelsea mabao 94 katika mechi 216.
Ancelotti ametamka: ‘Ni mtu muhimu kwetu. Tunataka aendelee kucheza hapa.”
Ndugu wa Riise atua Fulham
Mchezaji wa Kimataifa wa Norway ambae ni Kiungo, Bjorn Helge Riise, 26, amejiunga na Fulham kwa mkataba wa miaka mitatu na kwa dau ambalo halikutangazwa.
Bjorn Helge Riise, ambae Kaka yake John Arne Riise alicheza Liverpool kwa miaka mitano, anatokea Klabu ya Lillestrom na akiwa Fulham ataungana na Wachezaji wengine kutoka Norway, Brede Hangeland na Erik Nevland.
FIFA yaipiga Ivory Coast faini!
FIFA imekipiga Chama cha Soka cha Ivory Coast faini ya Dola Elfu 47 kufuatia uchunguzi kuhusu vifo vya Mashabiki 20 waliokufa mjini Abidjan kwenye Uwanja wa Felix Boigny mwezi Machi mwaka huu wakati Ivory Coast ilipokuwa ikicheza na Malawi kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia na kushinda mabao 5-0.
FIFA pia imetoa Dola Elfu 96 ili kuzisaidia Familia za Wafiwa.
Vilevile FIFA imetaka hatua za kusalama zichukuliwe kabla ya mechi ijayo itakayochezwa hapo Abidjan kati ya Ivory Coast na Burkina Faso mwezi Septemba ikiwa pamoja na kutoruhusu Washabiki zaidi ya 20,000 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 34,000.
Hatua nyingine ni kuweka vizuizi mita 200 kuzunguka nje ya uwanja ili kuzuia watu wasio na tiketi kuvamia uwanja kwani hilo ndilo lilikuwa chanzo cha watu kufa.

No comments:

Powered By Blogger