Sakata la John Terry laendelea, Lampard aongeza mkanganyo!!!
Kiungo wa Chelsea, Frank Lampard, ameongeza mkanganyiko kuhusu hatima ya Nahodha wao John Terry pale alipokiri hajui kama Terry anabaki au anaondoka huku Meneja wa Manchester City Mark Hughes, Klabu inayodaiwa ndio inamzuzua Terry, kudai kuwa wao bado wana imani kubwa Terry atakwenda Manchester.
Ingawa Chelsea yenyewe, ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Peter Kenyon na Kocha mpya Carlo Ancelotti, wameng’ang’ania Nahodha wao atabaki hakuna lolote Terry mwenyewe amesema kuhusu utata huu.
Lampard ametamka: ‘Sijui mwenyewe anataka nini. Kila mtu klabuni anataka abaki. Lakini watu wasimlaumu. Watu lazima waheshimu uamuzi wake kuchagua.'
Wakati huo huo, Meneja wa Manchester City, Mark Hughes, amekiri kuwa bado ana matumaini ya kumnasa John Terry ingawa Chelsea wameshaigomea ofa moja rasmi ya Man City.
Hughes anasema: ‘Ni Mchezaji wa hali ya juu. Bado hatujafikia pale tunaweza kukata tamaa hatumpati.”
Rooney: ‘Mzigo wa magoli ni kwangu, Berbatov na Owen!’
Wayne Rooney, akiwa ziarani na Timu yake Manchester United huko Asia, mbali ya kukubali kuna kazi kubwa ya kuziba pengo la Ronaldo na Tevez waliohama ambao kwa pamoja waliifungia Man U jumla ya mabao 41 msimu uliopita, anaamini pengo hilo haliwasumbui yeye, Berbatov na Owen.
Rooney vilevile amesema hawamlaumu Ronaldo kwa kuondoka kwani alikuwa mtumishi bora kwa Klabu hiyo kwa miaka 6 aliyodumu na amekiri kuwa yeye na Ronaldo wanaelewana sana.
Rooney anasema: ‘Kuondoka kwa Ronaldo kunafanya tuliobaki kufunga magoli mengi zaidi. Hatumlaumu Ronaldo kwa kuondoka.’
Kuhusu Tevez, Rooney ametamka: ‘ Ni rafiki yangu! Alikuwa akinifundisha maneno mengi ya matusi ya Kihispania! Ni bahati mbaya tulishindwa kurekebisha mkataba wake. Nadhani watu wengi watazungumza mengi kuhusu kuhamia kwake Man City lakini mimi sisemi chochote.’
Rooney mwenyewe amekiri kuwa endapo atachezeshwa kama Sentafowadi badala ya kupangwa pambeni au nyuma ya Sentafowadi atamudu kufunga mabao mengi sana.
Mara nyingi kwenye Kikosi cha Manchester United, Rooney hucheza kama mtu wa kumsapoti Mshambuliaji mkuu akiwa ama nyuma yake au pembeni yake kitu kilichokuwa kikimfanya awe mlishaji na si msifungaji.
Lakini Rooney amekiri suala hilo hawajaongea na Bosi wake Sir Alex Ferguson.
Rooney anasema: ‘Kila mtu anajua nipo hatari nikicheza Sentafowadi! Unafanya kazi kidogo, huzunguki mno uwanjani na unapata nafasi nyingi za kufunga!’
No comments:
Post a Comment