Monday, 20 July 2009

Sir Alex Ferguson: ‘Kuondoka Ronaldo ni pigo kwetu! Yeye ni bora kupita Kaka na Messi!’
-Man City sio tishio kwetu!

-Tishio bado Chelsea, Liverpool, Arsenal!
Meneja wa Manchester United Alex Ferguson ametamka kuondoka kwa Cristiano Ronaldo ni pigo kubwa kwa Mabingwa hao.
Ferguson amesisitiza: ‘Ni pigo kubwa! Sina cha kusema ila kumsifia kijana Yule! Kwa vyovyote vile yeye ni Mchezaji Bora Duniani! Ni bora kuliko Kaka na Messi! Yuko mbali sana kupita hao!’
Akiwageukia Mahasimu wao wa jadi, Manchester City, Klabu ambayo ni jirani zao mjini Manchester, Sir Alex Ferguson amekiri yeye pamoja na dunia nzima ya soka inashangazwa na jinsi wanavyonunua Wachezaji kwa bei mbaya.
Manchester City juzi tu wamemnunua Mshambuliaji wa Arsenal Emmanuel Adebayor kwa dau linalokadiriwa kuwa Pauni Milioni 25 na atajumuika na Wachezaji wengine wapya Gareth Barry, Roque Santa Cruz na Carlos Tevez.
Akiongea akiwa Kuala Lumpur, Malaysia ambako Man U wako ziarani Asia, Ferguson amenena: ‘Uhamisho wao wote waliofanya hawawezi kutupa ushindani labda kwenye kurasa za nyuma za Magazeti! Wao watashinda kwenye magazeti kwani kila siku zipo hadithi za ununuzi wao! Washindani wetu wakubwa bado ni Chelsea, Liverpool na Arsenal!’
Ferguson amesema itakuwa vigumu sana kwa Manchester City kushinda chochote licha ya kununua Wachezaji kwa sababu wamenunua Wachezaji wenye majina na tena sasa wana Washambuliaji 10 na amekiri hao ni wengi mno.
Ferguson ameongeza kwa kusema ameongea na baadhi ya Mameneja wenzake wa Ligi Kuu na wamejiuliza Man City watampanga nani na kumwacha nani, na yupi utamwambia hachezi.
Ferguson, akitafakari, alitamka: ‘Siwezi kusema kati ya Chelsea na Liverpool ipi ni timu ngumu zaidi kwani kila timu ni wazoefu! Arsenal wana kazi kubwa kuendeleza timu hasa baada ya kumuuza Adebayor. Pia hawana pesa kama za Chelsea na Liverpool. Jinsi Wenger atakavyoendeleza timu yake ndio mtihani wao mkubwa!’
‘Lakini…’ Ferguson akaongeza. ‘…..kitu kimoja tunachojua kuhusu Arsenal ni kuwa watakuja na soka bora kabisa! Watapata nafasi na ni rahisi kujijenga upya na kuleta ushindani!’
Ferguson akamalizia kwa kuigusa historia: ‘Tumekuwa Mabingwa mara 3 mfululizo na katika historia ya England hakuna Timu iliyokuwa Bingwa mara 4 mfululizo! Lyon huko Ufaransa wamechukua mara 7 mfululizo, Dynamo Kiev mara 9 na pia Celtic na Rangers! Dinamo Berlin ya ile Ujerumani Mashariki zamani walichukua mara 11! England huwezi kupata hilo!’
Sir Alex Ferguson akahitimisha: ‘Naongoza Klabu yenye falsafa sahihi. Nimepata wakati murua hapa. Kila mechi ya nyumbani Old Trafford kuna Mashabiki 76,000 wanatizama mechi laivu uwanjani hivyo siwezi kuijali Timu nyingine jirani hata wakifanya chochote!’

No comments:

Powered By Blogger